
ALIYEKUWA Kocha wa KenGold, Omary Kapilima, yupo katika mazungumzo ya kukiongoza kikosi cha B19 zamani kikifahamika kwa jina la Tanesco, baada ya timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu kutokuwa na mwenendo mzuri kwenye Ligi ya Championship.
Taarifa ambazo Mwanaspoti lilizipata, zinaeleza Kapilima aliyewahi kufundisha na kuchezea timu mbalimbali zikiwemo za, Majimaji, Yanga na Mtibwa Sugar, ameanza mazungumzo hayo na yamefikia hatua nzuri, hivyo, kilichobaki ni mambo madogo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kapilima amesema baada ya kumaliza mkataba wake na KenGold aliamua kuchukua muda wa kupumzika kwanza hivyo, kama kutakuwa na taarifa zozote ataziweka wazi, japo amekiri ni kweli zipo timu mbalimbali zinazomhitaji.
“Kwa sasa nimeamua kupumzika kwanza baada ya kipindi kirefu kilichobeba changamoto nyingi, ni uamuzi wa kwangu binafsi, ingawa muda siyo mrefu mashabiki na wadau wangu wataniona tena nikiwa na timu nyingine hivi karibuni,” amesema Kapilima.
Uongozi wa B19 unamhitaji Kapilima na tayari wawakilishi wake wamefanya mawasiliano hayo kwa lengo la kwenda kukinusuru kikosi hicho kilichochapwa mechi tano mfululizo za Ligi ya Championship, ikiwa chini ya kocha mkuu wa sasa, Babou Salim.