
Iran imelaani vikali mauaji yanayoendelea kufanywa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina pamoja na ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baghaei, amesema Jumapili kuwa kuendelea kwa mzingiro wa Gaza, sambamba na vizuizi vya kuondoa vifusi na kujenga upya miundombinu ya afya na huduma muhimu, kumezidisha mgogoro wa kibinadamu katika eneo hilo lililozingirwa, hususan katika hali ya baridi na mvua kubwa.
Baghaei alitaja vitendo hivyo kuwa ni sehemu ya “sera ya mauaji ya kimbari” dhidi ya wananchi wa Palestina.
Kwa mujibu wa Idara ya Ulinzi wa Raia ya Gaza, mahema kadhaa yaliyokuwa yakihifadhi familia zilizopoteza makazi katika eneo la Al-Mawasi, Khan Younis, yalifurika maji baada ya mvua kubwa na upepo mkali kwa siku tatu mfululizo.
Aidha, Baghaei amewalaumu walowezi wa Kizayuni kwa kuendeleza mashambulizi katika Ukingo wa Magharibi, ikiwemo kukiuka heshima za maeneo matakatifu kama Msikiti wa Al-Aqsa na Msikiti wa Ibrahimi, pamoja na kuwakamata na kuwatesa Wapalestina kiholela.
Amesisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa ina jukumu la kisheria na la kimaadili kusitisha uhalifu unaofanywa na utawala wa uvamizi.
Baghaei ameongeza kuwa hali ya Ukingo wa Magharibi ni mwendelezo wa “sera ya ukoloni ya kuteketeza” ambayo imesababisha mauaji ya maelfu ya raia wa Gaza katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Msemaji huyo pia amekosoa msaada wa kijeshi na kisiasa unaotolewa na Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya kwa Israel, akisema unawafanya washiriki wa moja kwa moja. Amesisitiza haja ya kukomesha hali ya kutowajibika kwa wahalifu wa vita na wanaohusika na mauaji ya kimbari.
Licha ya kile kinachoitwa kusitisha mapigano tangu Oktoba, vikosi vya Israel vimeendelea kushambulia Gaza mara kwa mara, na kusababisha vifo vya mamia ya Wapalestina katika wiki chache zilizopita.
Zaidi ya asilimia 80 ya majengo Gaza yameharibiwa, na kuacha sehemu kubwa ya eneo hilo kuwa lisiloweza kukalika.
Hali ya Gaza inatarajiwa kuwa ya maafa zaidi wakati huu wa msimu wa baridi. Misaada inayoingia imeendelea kuwa ya taratibu na isiyotosha kutokana na vizuizi vilivyowekwa na Israel.