
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio lililoandaliwa na Marekani la kuanzisha Kikosi cha Kimataifa cha Kurejesha Utulivu (ISF) katika Ukanda wa Gaza.
Azimio hilo, lililopitishwa Jumatatu, linaunga mkono mpango wa Rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu Gaza na kuidhinisha kuundwa muungano wa kulinda amani ambao utajumuisha nchi zenye Waislamu wengi kama vile Misri, Indonesia na Azerbaijan.
Azimio hilo limepingwa na harakati na makundi ya kupigania ukombozi ya Palestina. Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imepinga vikali azimio hilo, ikisema kwamba linalazimisha usimamizi wa kimataifa katika eneo hilo la Palestina. Taarifa iliyotolewa na Hamas imesema azimio hilo la UN halikidhi matakwa na haki za kisiasa na kibinadamu za watu wa Palestina.
Harakati hiyo imesisitiza kwamba kikosi chochote cha kimataifa kinapaswa kipelekwe kwenye mipaka ya Gaza pekee ili kufuatilia usitishaji mapigano chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.
“Kukipa kikosi cha kimataifa majukumu ndani ya Ukanda wa Gaza, ikiwa ni pamoja na kupokonya silaha za makundi ya mapambano, kunakipokonya sifa ya kutopendelea upande wowote, na kukifanya sehemu ya mzozo kwa niaba ya utawala vamizi,” imesema taarifa ya Hamas.
Serikali ya Marekani ilisambaza rasmi rasimu ya azimio hilo kwa wanachama 15 wa Baraza la Usalama wiki iliyopita. Rasimu hiyo ilipendekeza mamlaka ya miaka miwili kwa chombo cha utawala wa mpito na kikosi cha kimataifa cha kurejesha utulivu.
Russia, China na baadhi ya mataifa ya Kiarabu yalipinga pendekezo hilo, yakitaja wasiwasi kuhusu bodi ambayo bado haijaanzishwa itakayosimamia eneo hilo kwa muda na kutokuwepo jukumu lolote la mpito kwa Mamlaka ya Palestina.