
Dar es Salaam. Msafara wa kwanza wa kikosi cha Yanga umeondoka jijini Dar es Salaam leo Novemba 18, 2025 ukielekea Visiwani Zanzibar tayari kwa maandalizi ya mwisho wa mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya AS FAR Rabat mwishoni mwa wiki hii.
Yanga itakutana na AS FAR Rabat ya Morocco kwenye mchezo huo, utakaopigwa Novemba 22, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Visiwani humo.
Katika msafara huo, wameondoka na wachezaji ambao hawakuitwa katika timu za taifa ambao walikuwa wakiendelea na mazoezi chini ya kocha wao Pedro Goncalves.
Wachezaji pekee ambao wameongezeka kwenye msafara huo ni wale watatu ambao walikuwa kwenye timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Aidha Kocha wa Yanga Goncalves amesema kundi lingine la wachezaji waliokwenda timu mbalimbali za taifa watajiunga na timu hiyo moja kwa moja Visiwani humo.
“Tunaondoka kama kundi la kwanza wengine wataungana nasi kulekule. Uongozi umenihakikishia utafanya kila linalowezekana wafike kwa wakati,”amesema Goncalves huku akigoma kuzungumzia zaidi maandalizi yao.
Wakati Yanga ikienda hivyo Zanzibar, wenzao wa AS FAR Rabat watatua Zanzibar kesho tayari kwa mchezo huo ikiwahi kwa siku tatu kabla.
Mara ya mwisho kwa Yanga kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, iliibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya CBE ya Ethiopia.