Ujerumani na Uholanzi zimeongezeka katika orodha ya timu zilizofuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya jana kuibuka na ushindi katika mechi zao za nyumbani.

Katika Uwanja wa Red Bull Arena jijini Leipzig, wenyeji Ujerumani waliibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Slovakia uliowafanya wajihakikishie uongozi wa kundi A na kufuzu Kombe la Dunia wakifikisha pointi 15.

Mabao sita ya Ujerumani katika mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki wapatao 40,120 yalifungwa na Leroy Sane aliyepachika mawili kama ilivyokuwa kwa Ridle baku huku mengine yakiwekwa kimiani na Nick Woltemade na Serge Gnabry.

Uholanzi ilijihakikishia uongozi wa Kundi G baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 mbele ya Lithuania ambao umewafanya wafikishe pointi 20.

Mabao ya Uholanzi katika mchezo huo wa jana uliochezwa katika Uwanja wa Johan Cruijff Arena jijini Amsterdam yalifungwa na  Tijjani Reijnders, Cody Gakpo, Donyell Malen na Xavi Simons.

Kufuzu kwa Uholanzi na Ujerumani kunafanya sasa idadi ya timu ambazo tayari zina tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia mwakani huko Marekani, Mexico na Canada kufikia 34.

Ni timu 14 tu ambazo sasa zinasubiriwa ili zitimize idadi ya timu 48 ambazo zitashiriki mashindano hayo yenye thamani na mvuto mkubwa zaidi duniani katika ngazi ya timu za taifa.

Timu 34 ambazo tayari zimeshafuzu Kombe la Dunia 2026 ni Algeria, Cape Verde, Misri, Ghana, Ivory Coast, Morocco, Senegal, South Africa, Tunisia, Canada, Mexico, Marekani, Australia, Iran, Japan, Jordan, Qatar, Saudi Arabia, Korea Kusini, Uzbekistan, Croatia, England, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Norway, Ureno, New Zealand, Argentina, Brazil, Colombia, Ecuador, Paraguay na Uruguay.

Matokeo ya mechi za jana kufuzu Kombe la Dunia

Jamhuri ya Czech 6-0 Gibraltar
Ujerumani 6-0 Slovakia
Malta 2-3 Poland
Montenegro 2-3 Croatia
Uholanzi 4-0 Luthuania
Ireland Kaskazini 1-0 Luxembourg

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *