
Hii ni baada ya shambulizi la droni mapema kumuuwa mtu mmoja na kuwajeruhi wengine kadhaa, wakiwemo wanafunzi waliokuwa ndani ya basi. Wimbi hilo jipya la mashambulizi lilijiri siku moja baada ya shambulizi la angani kuwauwa watu 13 katika kambi ya wakimbizi ya Kipalestina ya Ein el-Hilweh. Lilikuwa shambulizi kali zaidi la Israel nchini Lebanon tangu makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah mwaka mmoja uliopita. Israel inadai kuwa Hezbollah wanajipanga upya.
Wakati huo huo, Israel imeripoti kuwa askari wake walifyatua makombora kusini mwa Gaza. Maafisa wa afya katika Ukanda huo wamesema mashambulizi ya Israel yaliwauwa kiasi ya Wapalestina 25. Kwingineko, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitembelea eneo lisilo na shughuli za kijeshi ndani ya Syria ambalo Israel ililikamata mwaka jana.