Nchini Mali, Kundi linalodai Kuunga Mkono Uislamu na Waislamu (JNIM), linalohusishwa na Al Qaeda, limetoa video mpya siku ya Jumanne jioni, Novemba 18, likizungumzia, miongoni mwa mambo mengine, vikwazo vilivyowekwa mapema mwezi Septemba dhidi ya uagizaji wa mafuta.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Ikiwa mwangalifu kutokuza propaganda za wanajihadi, lakini ikiendelea na dhamira yake ya kutoa taarifa, RFI inachambua taarifa hizi za hivi karibuni ambapo kundi la wanajihadi linakosoa mamlaka ya Mpito, linajaribu kuwashawishi Wamali, na kutangaza kuimarishwa kwa vizuizi hivyo.

Nchini Mali, msemaji wa JNIM kwanza anajaribu kudhalilisha mamlaka ya Mpito, akiituhumu kwa ulaghai. Kulingana na Nabi Diarra, anayejulikana pia kama Abou Houzeifa Al-Bambari, jeshi lililoko madarakani linahimiza vijiji kufanya makubaliano ya ndani na JNIM katika maeneo yaliyo nje ya udhibiti wa jeshi, kisha kushambulia vijiji hivi, likiwatuhumu kushirikiana na wanajihadi.

Katika miaka ya hivi karibuni, makubaliano kama hayo yameongezeka, hasa katika eneo la kati la nchi, kwa idhini ya kimyakimya ya idara za usalama za serikali ya Mali. Operesheni za kijeshi na unyanyasaji dhidi ya raia pia zimeongezeka. Wakati huo huo, maeneo yanayokataa kuingia katika makubaliano kama hayo yanakabiliwa na vizuizi vya JNIM—hakuna kinachoweza kuingia au kutoka—na hivyo kusababisha mateso makubwa kwa wakazi.

Msemaji wa JNIM pia anadai kwamba mamlaka inajadiliana kuhusu kuachiliwa kwa mateka wa kigeni, lakini si kwa wanajeshi wa Mali wanashikiliwa. Katika wiki za hivi karibuni, mateka mmoja wa Falme za Kiarabu aliachiliwa, na mateka wengine wa kigeni waliachiliwa kabla ya mateka huyo wa Falme za Kiarabu kuachiliwa. Raia kadhaa wa Mali pia wameachiliwa, ikiwa ni pamoja na meya wa Konna, mwishoni mwa mwezi wa Oktoba.

Hofu yatanda

Nabi Diarra kisha anajaribu kuhalalisha marufuku iliyowekwa mapema mwezi Septemba kuhusu uagizaji wa mafuta na udhibiti ulioongezeka kwenye barabara zinazoelekea Bamako, ambazo sasa zinauweka katika matatizo mji mkuu na maeneo mengine ya Mali. Msemaji wa JNIM kisha anajivunia athari za kizuizi hiki kwa raia: watu wengi wamepunguza kwenda kwenye vilabu vya usiku, wanawake wengi wanaonekana wakivaa hijabu katika barabara mbalimbali nchini… Yote haya ni kweli lakini raia wanalazimika kufanya hivyo kwa hofu na uoga na hayaonyeshi kwa vyovyote vile uungaji mkono wa raia kwa malengo ya JNIM.

Wanajihadi wanawatishia tena Wamali wanaoshirikiana na jeshi au wanaopambana nao moja kwa moja kwa kisasi cha vurugu, kuanzia na wawindaji wa jadi wa Dozo. Na kutaja mfano wa hivi karibuni wa Loulouni, katika eneo la Sikasso, ambapo wanajihadi walishambulia Wadozo waliokuwa wakijaribu kuwapinga. Mwanzoni mwa mwezi, JNIM ilimuua hadharani mwanablogu  Mariam Cissé, ambaye alikuwa ameelezea uungaji mkono wake kwa jeshi la Mali katika jimbo la Timbuktu. Mauaji haya yalisababisha wimbi la hasira na uzalendo kote nchini.

Kuimarishwa kwa kizuizi

Hatimaye JNIM imetangaza kuimarishwa kwa kizuizi hicho, ambacho sasa kitaenea hadi kwa kampuni zote zinazosafirisha mafuta. Kuhusu madereva wa malori ya mafuta, sasa watashughulikiwa na JNIM kama jeshi: hakutakuwa na wafungwa tena. Ikumbukwe kwamba tangu mwanzoni mwa mwezi Septemba, madereva wengi waliuawa na wengine kukamatwa.

Wiki iliyopita, mamlaka ya mpito ya Mali ilitangaza hatua za usaidizi: watoto wa madereva wa malori waliouawa katika mashambulizi hayo watakuwa jicho la taifa, na madereva waliojeruhiwa watapata huduma ya matibabu bila malipo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *