Dar es Salaam. Msimu huu wa 2025/2026 ni wa pili kwa mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube tangu alivyotua Jangwani msimu uliopita wa 2024/2025 akitokea Klabu ya Azam ambako alidumu kwa takribani misimu minne. Nyota huyo wa Kimataifa kutoka Zimbabwe aliwasiri kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara mwaka 2020 kujiunga na matajiri wa Chamazi akitokea kwenye Klabu ya   Highlanders FC ya kwao Zimbabwe.

Katika msimu wake wa kwanza wa 2020/2021 ulikuwa bora kwa nyota huyo baada ya kupachika mabao 14 katika Ligi Kuu, rekodi ambayo hadi sasa hajawahi kuifikia kwani katika msimu uliopita alimaliza kwa kufunga mabao 13 akiwa na Yanga. Msimu uliofuata wa 2021/2022 haukuwa bora kwakwe kwani alifunga bao moja tu, na hii ni kutokana na majeraha aliyokuwa anapata mara kwa mara ambayo yalimfanya muda mwingi kuwa nje ya Uwanja.

Msimu wa 2022/2023 alirejea tena katika Ligi Kuu huku safari hii akifunga jumla ya mabao 11 ndani ya msimu mzima wakati msimu wa 2023-2024 alifunga mabao saba kwani msimu huo pia aliandamwa na majeruhi baadhi ya nyakati. Hadi anaondoka Azam FC kwenda kujiunga na Yanga msimu uliopita, Dube alikuwa amefunga jumla ya mabao 33 katika Ligi Kuu.

ALIVYOIANZA MISIMU YANGA

Katika msimu uliopita wa 2024/2025 Dube alianza rasmi msimu wa Ligi Kuu ya NBC akiwa na jezi ya Wananchi, Yanga ambao walimpa matumaini makubwa ya kuweza kufanya makubwa kwenye timu kutokana na uwezo wake ambao alionyesha alipokuwa na Azam FC. Lakini kadri siku zilivyozidi kwenda, mambo yalianza kuwa magumu Jangwani baada ya kuonyesha kiwango cha chini katika michezo takribani 14 ya mashindano yote mwanzoni mwa msimu ambayo alicheza pasipokupata bao lolote.

Baada ya kuonyesha kiwango cha chini baadhi ya mashabiki wa Yanga walianza kumkosoa huku wengine wakimkatia tamaa wakionyesha kutoridhina naye, lakini wapo wengine ambao walisubiri kuona hatma ya mshambuliaji huyo itafikia wapi ndani ya Yanga ambayo kwa wakati huo ilikuwa na washambuliaji wengine hatari kama Clement Mzize na Kennedy Musonda.

ALIVYOANZA KUWASHAMOTO

Kama ambavyo hatujui siku wala saa ya kuja kwa mashihi ndivyo ambavyo Wananchi hawakujua ile siku ambayo Dube angerejesha makali yake. Hata hivyo, siku hiyo ilikuwa ni Desemba 14, 2024 ambapo Dube aliingia katika mchezo akitokea benchi dakika ya 62 akichukua nafasi ya Kennedy Musonda katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga mpaka muda huo ilikuwa nyuma kwa bao moja ambalo lilifungwa na Cheick Fofana dakika ya 41 kipindi cha kwanza.

Hadi kufikia dakika ya 90 Wananchi walijua wamepoteza mchezo ule huku zikiongezwa nne za nyongeza kutamatisha pambano hilo lililokuwa la kukata na shoka. Lakini pasipokutegemea katika dakika za majeruhi Prince Dube aliifungia Yanga bao la kusawazisha baada ya kipa wa TP Mazembe, Alioune Faty kuutema mpira uliokuwa umepigwa na Clatous Chama ambaye naye aliingia dakika ya 77 kuchukua nafasi ya Duke Abuya.

Na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa Dube kuanza makali ya kufumania nyavu kwani bao alilofunga dhidi ya TP Mazembe lilikuwa la kwanza kufunga baada ya kukaa siku 91 bila kupachika mpira wavuni.

Baada ya kumalizana na TP Mazembe mchezo uliofuata ulikuwa wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Yanga ilipoikaribisha Mashujaa United. Katika mchezo huo Dube aliendelea kuthibitisha makali yake wakati huu akifunga mabao matatu (Hat-trick) na kuipatia Yanga pointi tatu muhimu baada ya mchezo kumalizika kwa ushinda wa mabao 3-2.

Katika mchezo huo Dube aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Ligi Kuu katika msimu uliopita kufunga mabao matatu (Hat-trick) huku na yeye akifunga mabao kwa mara ya kwanza tangu ajiunge Yanga baada ya kucheza mechi 11 za Ligi Kuu bila kutikisa nyavu. Kwanzia hapo mashabiki wa Yanga walirudisha imani yao kwa Dube ambaye alimaliza msimu akiwa amehusika katika mabao 21 ambapo alifunga 13 na kutoa pasi za mwisho nane kiwango ambacho kilimfanya aendelee kusalia kwenye viunga vya Jangwani.

MAMBO MAZURI

Kama ilivyokuwa katika msimu uliopita ndivyo mambo yalivyoanza msimu huu, Dube akionekana kuwa mchezaji anayekosa nafasi nyingi za wazi, lakini juzi aliwafurahisha mashabiki wa Yanga baada ya kufunga bao muhimu kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya AS FA Rabat kwenye mchezo wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika likiwa ni la pili kwake kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika

baada ya kufunga tena kwenye ushindi wa 0-3 ugenini Wiliete ya Angola.

TATIZO LIKOWAPI

Hadi sasa Yanga imecheza michezo minne ya Ligi Kuu na katika michezo hiyo, Dube amecheza yote kwa dakika takribani 180 kwani alicheza mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Pamba Jiji kwa dakika 21, Mbeya City dakika 10, Mtibwa Sugar dakika 73 na KMC dakika 76. Hali hiyo imewafanya baadhi ya mashabiki wa Yanga kumtolea unyonge mshambuliaji huyo hasa baada ya kukosa nafasi za wazi katika mechi ya hatua ya awali raundi ya pili ya Ligi Mabingwa dhidi ya Silver Straikers ya Zambia mechi ambayo Yanga ilitinga hatua ya makundi kwa ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Dickson Job na Pacome Zouzoua.

Kocha wa zamani wa Klabu ya Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Charles Boniface Mkwasa maarufu kama Master alisema kuwa kiwango cha mchezaji kinaweza kuporomoka kwa sababu mbalimbali zikiwemo kutofanya mazoezi ya kutosha au kufanya mazoezi kupita kiasi;

“Kiwango cha mchezaji kinaweza kuporomoka kwa sababu anaweza kuwa hajafanya mazoezi ya kutosha au anaweza akawa anafanya mazoezi ya kuzidisha, kuna vitu vingi ambavyo ninaweza kuvielezea ambavyo vinaweza kusababisha kiwango cha mchezaji kushuka, kwa mchezaji kama Dube ambaye ni mzoefu kwenye ligi yetu anaweza kucheza lakini akawa hawezi kelewa makosa anayofanya uwanjani wala hawezi kuelezwa na mtu mwingine yoyote.

“Kwa hiyo anaweza kuwa anaendelea na makosa ili kutafuta njia ya kuwaaminisha wanachama na mashabiki wa Yanga lakini mashabiki nao wakionesha dalili za kutoridhika na kiwango chake licha ya kupewa nafasi ya kucheza kwa muda mrefu, hii inaweza kumfanya akapotea na kupoteza hali ya kujiamini, lakini siku moja anaweza kufanya mambo makubwa kama alivyofanya wikiendi iliyopita na wote mkasahau makosa yake yote.

“Lakini sababu zipo nyingi kwani pengine tatizo linaweza kuwa kwenye mtindo wa maisha yake jinsi anavyoishi, kwa mchezaji mzoefu kama yeye ni lazima ajitathmini mwenyewe mara baada ya kutoka kucheza uwanjani ili kujua kama amecheza vizuri au vibaya na iwapo amecheza vizuri anatakiwa ajue ni kitu gani amefanya kizuri na kama amecheza vibaya ajue ni kitu gani amefanya vibaya. Kwahiyo ni yeye mwenyewe kujua kama anacheza vibaya ili yale makosa yasijirudie katika mechi inayofuata na hiyo ndiyo kanuni ambayo lazima mchezaji ajitathmini mwenyewe,” amesema Boniface Mkwasa “Master”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *