
Dar es Salaam. Msanii mkongwe wa Bongofleva, Abbas Hamis ‘20 Percent’ amezungumzia nini maana ya a.k.a ya jina lake akidai ilitokana na uhusika wake katika familia, taifa na dunia akisisitiza hakujiita kwa bahati mbaya.
Mkongwe huyo aliyasema hayo wakati anazungumza na kituo cha redio cha Mjini FM, akieleza wakati anajiita jina hilo umri wake ulikuwa takriban miaka 20 ambapo ndipo alipofanya mambo mengi ya kimuziki.
“Katika dunia hii kuna Mungu aliye na asilimia 100, kuna malaika, mitume, matajiri, watu maarufu zaidi yangu. Kwangu kuna mimi katika familia, mimi katika taifa na mimi katika dunia. Katika dunia nina asilimia 20 ningeweza kujipa hata asilimia mbili, ila jina hilo lilikuja nikiwa ‘araundi’ miaka 20 na ndiyo muda niliofanya vitu vingi. Pia nilionyesha kujitambua nipo nafasi ipi katika dunia,” alisema 20 Percent.
Mtazamo wa mashabiki wake kuhusiana na kuona kashuka umaarufu wakimtofautisha na zamani kipindi alipopata tuzo tano za Muziki Tanzania, lakini msanii huyo alisema: “Kuwa juu kwangu ni sawa na nilivyo sasa, na nilivyo sasa ni sawa na kuwa juu.”
Aliwashauri wasanii wa kizazi cha sasa kuishi maisha ya kawaida hata kama wanamiliki vikubwa, jambo ambalo litawaweka salama katika jamii inayowazunguka.
“Sina tofauti na nilivyokuwa zamani na sasa. Niwe na pesa nisiwe na pesa hakuna atakayejua, kwani sikuwahi kuishi maisha ya kuigiza zaidi ya uhalisia wangu,” alisema 20Percent na kuongeza:
“Kuna watu ambao muziki upo ndani yao. Wapo wanaotaka kuwa wanamuziki sasa mimi muziki upo ndani yangu. Ndiyo maana situmii nguvu kubwa kufanya vitu nje ya kazi ilimradi watu waweke sikio kwa ajili yangu. Nikifanya kazi ndizo zinazonitambulisha kwao.”
20 Percent alisema hataki kuwa upande wa msanii yeyote au kundi fulani, badala yake anapenda kuwa kaka ili kukitokea changamoto awe mshauri. “Kuna albamu inakuja, lakini nitasema lini nitaitoa baada ya kuachia video ya Camera ambayo nimewashirikisha wasanii mbalimbali kama Joh Makini, Juma Nature hao ni baadhi tu,” alisema.