Novemba 20 kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine za Afrika kuadhimisha Siku ya Viwanda Afrika ambayo Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA, Disemba 1989) uliitangaza kupitia azimio namba A/RES/44/237.
Hii ilitokana na Mkutano wa Wakuu wa nchi wa Umoja wa Afrika (AU) enzi hizo ukijulikana kama “Organization of African Unity (O.A.U)” uliotoa uamuzi wa kuwa na Siku ya Viwanda ya Afrika katika Mkutano wake uliofanyika katika jiji la Addis Ababa Ethiopia, Julai, 1989.
Lengo kuu la siku hii ni kuongeza ufahamu na umakini kuhusu umuhimu mkubwa wa viwanda katika kukuza uchumi wa Afrika, kuongeza ajira, kuboresha maisha ya wananchi na kupunguza uhatarishi kutokana na athari mbalimbali.
Katika kulitekeleza hilo, Tanzania ikiwa nchi mwanachama wa AU inafanya juhudi mbalimbali za kuendeleza sekta ya viwanda ambapo kupitia Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) Serikali imekuwa ikitekeleza shughuli nyingi za kitaalamu ikiwemo tafiti ili kukuza sekta hiyo.
Katika maadhimisho ya mwaka huu, gazeti hili lilifanya mahojiano maalumu na Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Profesa Mkumbukwa Madundo Mtambo ambaye ameeleza kwa undani namna shirika hilo linavyosaidia juhudi za Serikali za kuendeleza sekta ya viwanda.
TIRDO imeadhimisha vipi Siku ya Viwanda Afrika mwaka huu?
TIRDO kupitia miradi yake mbalimbali kama vile mradi wa Utambuzi wa Viwanda, Rasilimali na Fursa za Uwekezaji (Industrial Mapping) unaoendelea katika mikoa ya Arusha na Manyara, imeendelea kutoa ufahamu kwa wenye viwanda na wenye uhitaji wa kuwekeza katika viwanda kwa kuwaelekeza malighafi zinapopatikana kwa wingi wa namna gani na vilevile kuelezea mazingira yanayowekwa na Wizara ya Viwanda na Biashara katika kuendeleza viwanda nchini.
Mpaka sasa zoezi la utambuzi limeshafanyika na kukamilika katika mikoa saba ambayo ni Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Tanga na Kilimanjaro. Mikoa mingine ni Shinyanga na Mwanza. Katika mikoa hiyo jumla ya viwanda vikubwa, vya kati na vidogo 23,150 vimefikiwa na kutambuliwa katika mikoa hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Twalib Abdalah akifungua semina ya mafunzo ya ukusanyaji wa taarifa za viwanda katika mikoa ya Arusha na Manyara. Semina hiyo ilitolewa na wataalam wa TIRDO Jijini Arusha.
Lengo ni kukamilisha taarifa zote katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara ili kama Taifa kuwe na taarifa halisi na sahihi juu ya viwanda nchini.
Ni shughuli zipi TIRDO imezifanya katika maadhimisho ya mwaka huu na zilikuwa na lengo gani katika kukuza sekta ya viwanda?
Katika kuadhimisha siku ya viwanda mwaka huu, TIRDO imefanya vitu mbalimbali ikiwemo kuonyesha teknolojia mbalimbali za kitafiti zilizofanywa ndani ya miaka kumi. Tafiti hizo ni kama vile:
Utafiti juu ya urejeshwaji wa bidhaa za plastiki (Plastic recycling technology) TIRDO imekuwa taasisi ya kwanza nchini kuanzisha teknolojia hii jambo ambalo limesaidia kupata malighafi na pia kuondoa taka ngumu mitaani.
Uzalishaji wa mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya vyakula pamoja na mabaki ya mazao mbali mbali kama vifuu vya nazi, vifuu vya chikichi pamoja na pumba za mpunga
Uanzishaji wa mfumo maalumu utakaowezesha kutoa taarifa sahii za viwanda nchini, mfumo huu unajulikana na NIIMS-National Industrial Infomations System.
Mfumo huu utasaidia katika kupata taarifa za viwanda kirahisi kwa ajili ya uwekezaji na pia kuonesha mapungufu katika mnyororo mzima wa uzalishaji wa viwanda nchini.
Wadau gani muhimu TIRDO inashirikiana nao katika utekelezaji wa shughuli zake na ushirikiano huo una mchango gani katika maendeleo ya viwanda?
Kwanza TIRDO inashirikiana kwa karibu na taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kama vile, SIDO, TEMDO, TBS, BRELA katika shughuli za kuendeleza viwanda. Mchango mmojawapo kwa maendeleo ya viwanda ni ushirikiano wa kuendeleza teknolojia kwa matumizi ya viwanda kati ya TIRDO, SIDO na TEMDO. Pili ni ushirikiano wa TIRDO na TBS kuhakikisha kuwa viwanda vyetu vinazalisha bidhaa bora zenye viwango vya kuweza kushindana katika soko la ndani na la kimataifa.
TIRDO imekuwa na mchango gani katika kusaidia viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kuboresha uzalishaji na ubora wa bidhaa?
Jukumu lingine la TIRDO ni kuhakikisha kuwa viwanda vya aina zote vinaendelea na kuzalisha bidhaa zilizo bora katika masoko yote, yaani soko la ndani na la kimataifa.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uhandisi wa TIRDO, Mhandisi Ramson Mwilangali (kushoto), akionyesha malighafi inayozalishwa katika karakana ya TIRDO inayotumika kuzalisha bidhaa za Plastiki. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Profesa Mkumbukwa Madundo Mtando na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti na Maendeleo (REPOA), Dk Donald Mmary.
Hivyo basi michango mikubwa ya TIRDO katika kusaidia viwanda vya aina zote ni ubunifu na uhaulishwaji wa teknolojia za viwanda kwa viwanda hivi, uboreshaji wa maabara za TIRDO kwa kupata Ithibati (Accreditation) ili viwanda viweze kutumia kuhakiki ubora wa bidhaa zao, utoaji wa mafunzo mbalimbali kama vile kuongeza thamani, uhakiki wa matumizi sahihi ya nishati viwandani, ukaguzi wa mitambo ya viwandani na ushauri katika uzalishaji viwandani.
Je, unaweza kuelezea miradi mikubwa ya utafiti au ubunifu inayotekelezwa na TIRDO kwa sasa ambayo inalenga kuchochea maendeleo ya viwanda nchini?
Kwa sasa TIRDO inatekeleza Mradi wa Utambuzi wa Viwanda, Rasilimali na Fursa za Uwekezaji (Industrial Mapping) kwa nchi nzima ambayo unaenda kuchochea maendeleo ya viwanda kwa kuweza kuainisha malighafi mbalimbali za viwanda, ujuzi wa wataalamu wa viwanda, changamoto na jinsi ya kuzitatua.
TIRDO imeanza kutekeleza Mradi wa Utambuzi wa Madini ya kimkakati (Critical Minerals) ambayo utaenda kubainisha madini na maeneo yaliko na kuweza kubainisha ni teknolojia gani na viwanda gani vya kuongeza thamani vya kuanzisha katika maeneo hayo.
TIRDO inatekeleza Mradi wa Matumizi bora ya Nishati (Energy Efficient) viwandani na katika majengo makubwa. Mradi huu umelenga kupunguza/kuboresha matumizi ya nishati yasiyo ya lazima ambayo itapelekea kuwa na gharama nafuu za uzalishaji.
TIRDO inaendelea kutekeleza Mradi wa Usimamizi wa ujenzi wa viwanda nchini ambao unachochea maendeleo ya viwanda nchini. Mfano TIRDO inasimamia kiwanda kikubwa cha bidhaa za ngozi, Kilimanjaro International Leather and Leather Products za mkoani Kilimanjaro.
TIRDO inaendelea kufanya tafiti za kuanzisha ujenzi wa viwanda, kuboresha viwanda vilivyopo ili kuongeza uwezo wa uzalishaji wa viwanda hivyo. Mradi wa Kitaifa wa Engaruka Soda Ash ni matokeo makubwa ya TIRDO katika kufanya tafiti za aina hizo za malighafi na kuendeleza ujenzi wa viwanda nchini.
Ni teknolojia au tafiti zipi zilizotokana na TIRDO ambazo zimefanikiwa kuleta mabadiliko halisi katika uzalishaji wa viwanda vya Tanzania?
Tafiti ya kubaini ubora na wingi wa madini ya Soda katika eneo la Engaruka ni tafiti kubwa kutoka TIRDO iliyowezesha Taifa kupata mwekezaji katika eneo hili ambapo wa sasa mazungumzo yanaendelea katika kuwekeza kwenye mradi huu.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uhandisi wa TIRDO, Mhandisi Ramson Mwilangali (kushoto), akionyesha malighafi inayozalishwa katika karakana ya TIRDO inayotumika kuzalisha bidhaa za Plastiki. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Profesa Mkumbukwa Madundo Mtando na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti na Maendeleo (REPOA), Dk Donald Mmary.
Teknolojia ya kuhakiki pasipo kuharibu Non Destructive Testing (NDT) imewezesha miradi mikubwa ya Serikali ya kimkakati kuendelea kwa ubora wa kimataifa, miradi ya SGR, bomba la gesi asilia Mtwara, mitambo ya viwandani kama vile “boilers”, “compressors” imeweza kuhudumiwa na teknolojia hii.
TIRDO kupitia maabara zake iliweza kubainisha upotoshaji wa viwango vya madini mbali mbali katika mradi mmojawapo wa nchi hivyo basi kupelekea nchi kuutazama mradi huo upya.
Pia TIRDO kupitia maabara hizo imeweza kubainisha ubora wa Makaa ya Mawe ya Tanzania na ikapelekea nchi kupiga marufuku ya uagizaji wa madini hayo toka nje ya nchi. Hii imepelekea uzalishaji wa Makaa ya Mawe kuongezeka, kuongezeka kwa mapato ya nchi na kuongezeka kwa upelekaji wa Makaa ya Mawe nje ya nchi (Export Trade).
TIRDO imechukua hatua gani kuhakikisha tafiti zake zinatumika na wawekezaji au wazalishaji badala ya kubaki katika makaratasi?
Kwa sasa TIRDO imebadilika sana katika kufanya tafiti zake. Tafiti za kishule hazipo tena TIRDO na kama zipo zinahusisha jamii kwa kuangalia tatizo lililopo kwa jamii husika na kufanya utafiti wenye kuleta jinsi ya kutatua tatizo hilo. Mfano utafiti ya kubaini ubora na wingi wa madini ya Soda katika eneo la Engaruka ni utafiti mkubwa kutoka TIRDO uliofanywa kwa kushirikana na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) uliyowezesha Taifa kupata mwekezaji katika eneo hili ambapo kwa sasa mazungumzo ya uwekezaji yanaendelea katika kuwekeza kwenye mradi huu.
Mtafiti na Mkufunzi wa Nishati Safi, Mhandisi Augunstino Masse (katikati, mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya nishati safi awamu ya pili yaliyofanyika Novemba 2025. Wengine ni washiriki wa mafunzo hayo wakionesha vyeti walivyotunukiwa mara baada ya kumaliza mafunzo.
Pia TIRDO kupitia utafiti uliofanywa kwa kushirikiana na wadau walioendelea wa kimataifa na maabara imeweza kubainisha ubora wa Makaa ya Mawe ya Tanzania na ikapelekea Serikali kupiga marufuku ya uagizaji wa madini hayo toka nje ya nchi. Hii imepelekea uzalishaji wa Makaa ya Mawe kuongezeka, kuongezeka kwa mapato ya nchi na kuongezeka kwa upelekaji wa Makaa ya Mawe nje ya nchi (Export Trade).
Yote hii inaonyesha jinsi TIRDO ilivyojisheheneza wataalamu na jinsi inavyokwenda na wakati kwa kuachana na tafiti za makaratasi na kuja na tafiti zenye tija na kutatua changamoto za wadau wake ndani na nje ya nchi.