
AISHI Manula usiku wa leo Jumatano Desemba 3, 2025 amekaa golini kwa mara ya kwanza akiidakia Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara baada ya kupita takribani siku 638.
Mara ya mwisho Manula kudaka mechi ya Ligi Kuu Bara ilikuwa Machi 6, 2024 akiwa Simba, akiruhhsu mabao mawili katika kichapo cha 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Baada ya hapo, hakudaka mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara wala mashindano yoyote ngazi ya klabu hadi leo akiibukia Azam iliyoikaribisha Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam na matokeo kuwa 0-0.
Siku hizo 638, ni sawa na mwaka mmoja, miezi minane na siku 28 ambapo Manula alikuwa akiishia benchi au jukwaani bila ya kuvuja jasho katika mechi za klabu.
Katika mechi ya leo ambayo Azam ilitengeneza nafasi nyingi lakini ikashindwa kuzitumia, Manula ameanza golini badala ya Issa Fofana aliyekaa benchi, huku Zuber Foba akikosekana kabisa.
Manula aliyerejea Azam msimu huu baada ya kumaliza mkataba akiwa na Simba alioitumikia kuanzia msimu wa 2017-2018 hadi 2024-2025, wakati akiwa hajacheza mechi yoyote ya mashindano tangu atue hapo, kikosi hicho kilikuwa kinawatumia makipa Zuberi Foba na Issa Fofana raia wa Ivory Coast aliyesajiliwa akitokea Al Hilal ya Sudan.
Matumaini ya Manula kurejea golini yalianza kuonekana Novemba 23, 2025 alipokaa benchi kwa mara ya kwanza wakati Azam ikilala mabao 2-0 mbele ya AS Maniema ya DR Congo ikiwa ni mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika kundi B aliyodaka Foba.
Katika kuonyesha matamanio ya kurejea golini, wakati Azam inajiandaa kuikaribisha Wydas katika mechi ya pili Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi iliyochezwa Novemba 30, 2025, Manula alinukuliwa akisema uzoefu na historia havitoshi kumfanya kocha ampe nafasi, bali ni kuonyesha uwezo kwenye uwanja wa mazoezi ili kumshawishi.
“Mazoezini ni sehemu pekee ya kumuonyesha mwalimu maana mpira ni mchezo wa wazi na historia haitoshi kumfanya anipe nafasi ya kucheza, bali ni jitihada ambazo anaziona na unavyopambana na anapokuona upo tayari.
“Kama nilivyosema nilikuwa napitia changamoto nyingi nilipokuwa, lakini sasa nimeweza kurejea na kuendelea kupambana kumuonyesha mwalimu kwamba kulingana na uzoefu niliokuwa nao lakini ukijumlisha na jitihada ninazozionyesha mazoezini basi itampa yeye sababu ya kuona kama natosha kupewa nafasi ya kucheza,” alisema Manula, hata hivyo mechi hiyo alidaka Foba, benchi akakaa Fofana, yeye akaishia jukwaani.
Wakati akipitia wakati mgumu wa kushindwa kupata nafasi ya kucheza ndani ya klabu kipindi yupo Simba, Manula aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024, zilizoandaliwa na Tanzania kwa kushirikiana na Kenya, Uganda kuanzia Agosti 2, 2025 hadi Agosti 30, 2025. Hata hivyo, hakucheza kwani Yakoub Suleiman alidaka zote.
Kabla ya hapo, Manula alicheza mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 dhidi ya Guinea, Novemba 19, 2024, licha ya kwamba alikaa muda mrefu bila ya kupata nafasi katika klabu, lakini aliyekuwa kocha mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman Morocco alimuita.
Msimu huu Azam ikiwa imecheza jumla ya mechi kumi za mashindano ambapo sita Kombe la Shirikisho Afrika na nne Ligi Kuu Bada, Foba ndiye amedaka mechi nyingi akifikisha tano, huku Fofana akidaka nne na Manula moja.
Katika Ligi Kuu Bara, Azam haijaanza vizuri msimu huu ikishinda mechi moja pekee dhidi ya Mbeya City kwa mabao 2-0, huku ikitoka sare tatu dhidi ya JKT Tanzania (1-1), Namungo (1-1) na Singida Black Stars (0-0).