Vijana wengi katika jiji la Tanga wamejikuta wakishindwa kufikia matarajio yao katika maisha kutokana na kukosa fursa. Hii imesababisha wengi kujikita kwenye kazi zisizo rasmi, ukulima mdogo na shughuli za uvuvi zisizokuwa endelevu.
Aidha, ufikiaji mdogo wa mifumo ya kifedha au mafunzo ya ujasiriamali, uwekaji wa akiba kwa vijana hao vilionekana kuwa changamoto na hivyo kuwafanya kushindwa kutekeleza shughuli endelevu za kiuchumi.
Pia, maelfu ya vijana katika jiji hilo wanakabiliwa na changamoto nyingine ikiwemo; ukosefu wa ajira, upatikanaji mdogo wa mikopo na ukosefu wa mawazo ya kibiashara ambayo yanaweza kuwasaidia kutokutegemea kuajiriwa. Katika jamii ambapo upatikanaji wa mitaji mara nyingi unarudisha nyuma maendeleo ya vijana wengi, Tanga nayo ni sehemu yenye changamoto hiyo.
Hapa ndipo unapoingia Mradi wa Mabadiliko ya Fikra na Ujasiriamali ambao ni sehemu ya awamu ya kwanza ya programu ya TangaYetu iliyoongozwa na Reconstructed Living Lab (RLabs). Mradi huu lengo lake sio tu kutoa mafunzo kwa vijana katika ujasiriamali, lakini pia kubadilisha jinsi wanavyojiona, kufikiri na kutumia uwezo wao.
Mbinu hii ilianza na utafiti wa kimsingi wa kutathmini fursa za biashara zinazofaa kwa vijana. Kisha zikaja warsha za uongozi za GROW, kambi za mafunzo ya ujasiriamali, mafunzo ya ujuzi wa kidijitali na vipindi vya mafunzo ya kuweka na kukopa kwa vijana.
Katika jamii zilizofikiwa na mradi huu, kuliundwa vikundi vya kuweka na kukopa vya kijamii kama vile Karange One na TUNDAUWA. Lengo lilikuwa ni kujenga mifumo ya kifedha inayoongozwa na kumilikiwa na vijana.
TUNDAUWA ilivyoleta uhuru wa kifedha kwa vijana katika ngazi ya jamii
Umoja wa Vijana TUNDAUWA ni kikundi cha kuweka na kukopa cha vijana chenye wanachama 21 wakijumuisha wanawake 16 na wanaume watano ambao wameunganishwa na dhamira ya pamoja ya ukuaji wa kifedha na kusaidiana. Kupitia kikundi hicho, wanachama huchangia mapato yanayotokana na kilimo, uvuvi na ujasiriamali.
Fedha hizi hutolewa kwa njia ya mkopo ili kuwasaidia wanachama kuwekeza katika miradi kama vile kilimo cha mihogo na mabwawa ya samaki. Mbinu hii inasisitiza uthabiti, uaminifu na mtaji wa jamii.
“Hii ni zaidi ya akiba bali ni kutengeneza fursa za kuwekeza katika siku zijazo. Jambo muhimu katika mpango huu ni dhana ya mabadiliko ya mawazo,” anasema Muweka Hazina wa TUNDAUWA, Rajabu S. Rajabu.
“Kikundi hiki kilianzishwa baada ya mafunzo yaliyotolewa chini ya TangaYetu kwani kabla ya ujio wa programu hiyo hatukujua tuanzie wapi,” anasema Time Khamisi Selemani, mwanachama wa TUNDAUWA.
Mwezeshaji na Msimamizi wa Mradi, Halima Ally Bughe anaeleza jinsi washiriki walivyojifunza kubadilisha mapato ya kawaida kuwa uwekezaji mkubwa. “Tuliwafundisha kuweka akiba kidogo kama Sh 100 na sasa wanakuza mitaji yao na kujitegemea.”
Wanachama wa kikundi cha TUNDAUWA wakiwa katika kikao cha kujadili maendeleo, ushirikiano na uwezeshaji wa vijana wa kikundi hicho.
Mwenyekiti wa kikundi cha TUNDAUWA, Rashid Khamisi Ibrahim amesisitiza azma ya kikundi hicho kwa kusema kuwa, “Tunataka kuongeza miradi kama vile kilimo cha mihogo na ufugaji wa samaki. Mawazo haya yanaweza kubadilisha kikundi chetu na jamii nzima.”
Karange one: Mhimili wa uwezeshaji wa kifedha kwa vijana
Karange One ni kikundi cha akiba na mikopo chenye wanachama wenye umri kati ya miaka 18 hadi 30. Kupitia shughuli za kiuchumi, kikundi hicho kimeonyesha hali ya kujitegemea na ustadi, kuunganisha rasilimali ili kusaidia matarajio ya mtu binafsi na ya pamoja.
Kama vilivyo vikundi vingine, Karange One inatumia njia za michango ya wanachama ambapo michango ya kila wiki ya wanachama inawawezesha kupata mikopo ambayo wanaitumia katika kupanua biashara zao na kukidhi mahitaji ya familia. “Nilitumia mkopo wa kikundi kujenga nyumba ya kisasa na mkopo mwingine ulinisaidia kuanzisha kikundi kingine cha Kijibweni One,” anasema Jafari Shali Rashidi, katibu wa kikundi.
Kwa Asia Mmaka Ramadhani ambaye ni Mweka hazina wa kikundi, Karange One ni zaidi ya pesa. “Nguvu zetu ziko katika umoja. Kwa pamoja, tunaweka akiba leo ili kujenga usalama wa kesho. Chochote kinachotokea katika maisha tunaweza kusaidiana wenyewe kwa wenyewe.”
Wanachama kama Fatuma Mwidadi Gau waligeuza mikopo midogo kuwa miradi ya kujiingizia kipato. Alinunua friji na kuanza kutengeneza na kuuza aiskrimu na juisi. Amina Ally, mwanachama mwingine, alitumia mtaji wake kupanua duka lake na kusomesha watoto wake. “Kikundi hiki kimekuwa cha kubadilisha maisha,” anasema Amina.
Mafanikio hupimwa kwa matokeo
Mbali na faida za kifedha, mafanikio makubwa zaidi yamekuwa katika kubadilisha mawazo na mitazamo. Kilichoanza kama vipindi vya mafunzo vilibadilika na kuwa shughuli za uchumi. Vikundi ambavyo hapo awali vilitegemea misaada kutoka nje sasa vinajenga uthabiti wao wenyewe, kupitia michango midogo midogo ya wanachama wake.
Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya vijana 1,036 walifikiwa, mamia ya biashara ndogo zilianzishwa, maelfu ya shilingi za Kitanzania ziliingizwa katika mzunguko kama mikopo ya vikundi. Hizi sio tu takwimu za kwenye makaratasi, bali ni ishara ya ujenzi wa uchumi imara na endelevu kwa jamii hizo.
Mafanikio ya Karange One na TUNDAUWA yanatoa taswira yenye nguvu kwamba maendeleo ya kiuchumi huanza na kujiamini na katika uwezo wa pamoja wa jamii. Hili ni funzo kwamba mifumo ya kifedha sio lazima iwe na sheria na taratibu nyingi ili kuwa na ufanisi bali inatakiwa ijengwe katika uaminifu.
Programu ya TangaYetu katika awamu yake ya pili, mfumo wake wa uwezeshaji kwa vijana unatoa funzo ambalo linatakiwa kuigwa katika miji yote ya Afrika la kuwawezesha vijana si tu kwa ujuzi, lakini kwa mifumo na nafasi ya kustawi.
“Vijana wanapokuwa na vifaa, ujuzi na maono ya pamoja, wanafanya mengi zaidi ya kukuza biashara,” anasema Halima msimamizi wa mradi kutoka RLabs.
Programu ya TangaYetu inafadhiliwa na Fondation Botnar na inatekelezwa na kampuni ya INNOVEX Development Consulting Limited kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga