
Mbeya. Katika kuhakikisha wataalamu vishoka wanadhibitiwa, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhandisi , Zena Ahmed amesema Serikali iko mbioni kutoa usajili kwa Bodi ya Wanajiosayansi Tanzania(TGS).
Hatua hiyo imetajwa kuiwezesha kusimamia , kuwasajili na kuthibitisha wataalamu ili kudhibiti watu wasio sahihi,vishoka ambao wanaweza kuleta madhara katika tafiti mbalimbali hususani za uchimbaji wa visima vya maji.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Desemba 3,2025,Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhandisi ,Zena Ahmed wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa TGS, uliofanyika mkoani hapa.
Mkutano huo umehusisha wataalamu,wanajiosayansi 4,000, kutoka Wizara mbalimbali ,Taasisi za Serikali na Vyuo vikuu.
“Lengo ni kuiwezesha bodi kuthibitisha na kuchuja watu wasio stahili kufuatia kuwepo kwa watu wanao jifanya wataalam kumbe sio mwisho wa siku wakaleta shida,”amesema.
Katika hatua nyingine amesema Serikali inatambua mchango mkubwa waTGS, katika ugunduzi na uendelezaji wa migodi ya madini ya aina mbalimbali sambamba na upatikanaji wa rasilimali za maji ardhini ,ugunduzi wa mafuta ,gesi na utafutaji wa nishati ya joto ardhini.
“Tunapo zungumzia utajiri wa rasilimali asilia kwa sababu tumeshuhudia namna sekta ya madini na wanajiosayansi wakiwa miongoni mwa msingi wa kuchangia asilimia 10 kwenye pato la Taifa,”amesema.
Wakati huo huo amesema mkutano huo wa mwaka wakajadili namna TGS, inavyoweza kuchangia kufanikisha Dira ya Maendeleo yaTaifa 2050,elimu kwa jamii kuhusiana na ajenda ya matumizi ya nishati safi na teknolojia za kisasa .
“Mkutano huu umekuja wakati nchi imetoka kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2025 na kuanza utekelezaji wa Dira ya mwaka 2050,sasa wataalamu tujadili namna bora ya kutoka kwenye matumizi ya nishati chafu na kugeukia nishati safi ili kufikia malengo ya Serikali na kuokoa maisha ya watanzania, “amesema.
Pia, amewataka kuisaidia Serikali kufanya tafiti za kina ardhini na kwenye miamba ili kubaini maeneo yanayo stahili kujenga makazi ya watu,uchimbaji wa madini, mafuta na gesi.
Kwa upande wake Rais wa Wanajiosayansi Tanzania (TGS), Prof Elisante Mshiu amesema mchango wao ni kuendeleza na kukuza migodi ya wachimbaji nchini na upatikanaji wa rasilimali za nishati ya mafuta na gesi.
Amesema wanaendelea kushirikiana na jumuiya za kimataifa na kikanda hususani Afrika,Kenya Uganda na nyingine nyingi lengo ni kunufaika na fursa mbalimbali.
Amesema pamoja na mchango wa ugunduzi wa rasilimali mbalimbali kuna changamoto ya kuzifanyia kazi licha ya kuanzishwa kwa bodi ya usajili ya wataalam katika nyanja mbalimbali.
“Ingawa kupitia Kamati tumepiga hatua kubwa katika kufanikisha suala hilo ,lakini tunaendelea kulifanyia kazi hivyo ili kuonekana mchango wetu tunaomba mchakato wa kusajili bodi ufikie mwisho ili kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa Endelevu 2050,”amesema.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Beno Malisa, Katibu Tawala Msaidizi, Viwanja, Biashara na Uwekezaji, Anna Mwambene amesema ufike wakati wataalamu kufanya tafiti za kina za hali ya udongo ili kudhibiti madhara hususani kwa wachimbaji wa madini.
“Utafiti wa kidiolojia ufanyike kwa tija kubwa kwenye maeneo ya miamba na ardhi ili kusaidia wachimbaji wadogo kutokana tamaa ili kuongeza wigo mpana katika sekta ya madini mkoani hapa,”amesema.
Amesema Mkoa wa Mbeya unashika nafasi ya pili kitaifa katika sekta ya madini ya dhahabu , hivyo kupitia mkutano huo wa wanajiosayansi uje na matokeo makubwa kufanya kupanda hadi kushika nafasi ya kwanza.
Kauli za wachimbaji.
Mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu Kijiji cha Saza Mkoa wa Songwe,Christopher Fredy amesema wanakabiliana na changamoto ya ukosefu wa vifaa maalum vya kufanya tafiti katika maeneo ya uzalishaji na kuomba Serikali ione namna ya kuwafikia.
“Tumekuwa tukichimba kwa mazoea kwa kutumia vipimo visivyo na uwezo mkubwa jambo ambalo linachangia uharifu wa mazingira kwa kuvamia maeneo mengi zaidi bila kufanikiwa,”amesema .