Huenda Malale Hamsini akawa Kocha Mkuu wa KMC siku chache zijazo akichukua nafasi ya Marcio Maximo ambaye anaelekea kuonyeshwa mlango wa kutokea na timu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni.

Habari kutoka chanzo cha ndani ya KMC kimeiambia Mwananchi Digital kuwa baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuachana na Maximo, timu hiyo itamtangaza Malale Hamsini kama Kocha Mkuu mpya.

“Mazungumzo na Malale Hamsini yapo katika hatua nzuri na ndiye kwa asilimia kubwa atachukua nafasi ya Maximo. Kwa sasa yapo masuala kadhaa ya kumalizana na Maximo kabla ya kutangaza kuachana naye.

“KMC ni timu ambayo iko chini ya taasisi ya kiserikali hivyo haiwezi kufanya maamuzi kwa kukurupuka, ndio maana inaonekana kama inachelewa kuachana na Maximo,” kimefichua chanzo hicho.

Malale Hamsini hivi karibuni alikuwa akiinoa Mbeya City ambayo iliamua kuachana naye kutokana na mwenendo usioridhisha kwenye Ligi Kuu msimu huu.

Kupoteza mechi ya nyumbani dhidi ya Namungo FC kwa bao 1-0, kulikoleza moto uamuzi wa uongozi wa Mbeya City kuachana na Malale Hamsini ambaye ndiye aliiongoza timu hiyo kupanda Ligi Kuu.

Katika mechi tisa ambazo Malale Hamsini aliiongoza Mbeya City msimu huu, timu hiyo ilipata ushindi katika michezo miwili, kutoka sare mbili na kupoteza mechi tano.

Mwenendo wa KMC chini ya Maximo umekuwa sio wa kuridhisha kutokana na idadi kubwa ya pointi ambazo imepoteza katika mechi tisa ilizocheza hadi sasa.

KMC imepata ushindi katika mechi moja tu huku ikitoka sare moja na imepoteza michezo saba kwenye ligi hadi sasa.

Matokeo hayo yameifanya KMC ishike mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi nne.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *