
Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesaini hati ya makubaliano na Kampuni ya Africa Global Logistics (AGL) kwa ajili ya usanifu, ujenzi na uendeshaji wa gati mpya tatu katika Bandari ya Bagamoyo.
Hati ya makubaliano (MoU) imesainiwa jana makao makuu ya mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa na Rais wa AGL, Philippe Labonne.
Mbossa alisema kusainiwa kwa hati ya makubaliano hayo ni ishara ya utayari wa kuanza kwa mradi wa bandari mpya ya Bagamoyo ambao kwa kuanzia AGL yenye makao makuu yake nchini Ufaransa, itaanza usanifu na ujenzi wa gati tatu mpya za kisasa kati ya 28 zinazotarajiwa kujengwa bandarini hapo.
Vilevile kutajengwa gati mbili mpya za kisasa katika Bandari ya Dar es Salaam.
“Tunategemea kuanza ujenzi wa gati mpya tatu katika Bandari ya Bagamoyo mapema Januari (2026) na pia tunawakaribisha wawekezaji wengine wa ndani na wa nje katika mradi huo. Lengo ni kuleta mapinduzi makubwa katika shughuli za kibandari nchini,” alisema Mbossa.
Kwa upande wake, Rais wa AGL, Labonne alisema wameamua kuingia makubaliano na TPA na kuwekeza Tanzania kutokana na kuwa nchi yenye amani, usalama, mazingira bora na tulivu ya uwekezaji iliyo sehemu sahihi kijiografia kwa sekta ya uchukuzi na kuwa lango la biashara kitaifa na kimataifa.
“Ninaamini Tanzania ni nchi inayokua kwa kasi kimaendeleo, ikiwa na mtaji mkubwa wa watu wakarimu na mtazamo chanya,” alisema na kuongeza:
“Pia ni lango la kuingilia nchi nyingi barani Afrika na kuyafikia masoko ya kimataifa, hivyo naamini ushirikiano huu utafungua mambo mengi, ikiwemo kutengeneza ajira ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.”
Mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo kwa gati mpya tatu utajengwa kwa miezi 36 (miaka mitatu).
Kampuni ya AGL imeelezwa na mamlaka kuwa imepata nafasi a kushirikiana na TPA katika ujenzi huo kutokana na uzoefu wake kama kampuni kubwa ya huduma za usafirishaji na logistiki.
Kwa nini Bandari ya Bagamoyo
Mradi wa Bandari ya Bagamoyo na Eneo Maalumu la Kiuchumi (BSEZ) ulianzishwa kwa lengo la kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam.
Melengo mengine ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji katika Afrika Mashariki na Kati.
Mikataba ya kuanza ujenzi ilisainiwa Oktoba 2015, ikipangwa kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi mwaka 2017.
Hata hivyo, tangu kipindi hicho mradi huu ulikumbwa na changamoto kadhaa zilizochangia kusuasua kwake.
Januari 2016, Serikali ilisitisha mradi huo kutokana na vipengele vya mkataba vilivyoonekana kuwa na masharti magumu.
Rais wa wakati huo, Hayati Dk John Magufuli, alieleza mkataba huo ulikuwa na vipengele visivyofaa, ikiwa ni pamoja na sharti la kutojenga wala kuendeleza bandari yoyote kuanzia eneo la Tanga hadi Mtwara.
Ahadi ya Rais Samia
Akiwa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwenye viwanja vya Polisi mkoani Pwani, Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mambo mengine, aliahidi kufufua na kutekeleza mradi wa Bandari ya Bagamoyo akisema itajengwa eneo la Mbegani na utakuwa na gati za kisasa zenye uwezo wa kupokea meli kubwa zaidi ya zile zinazoingia Bandari ya Dar es Salaam.
“Tunakwenda kuijenga Bandari ya Bagamoyo katika eneo la Mbegani. Bandari hii itakuwa na gati za kisasa na ndefu ambazo zitakuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa zaidi ya Bandari ya Dar es Salaam,” aliahidi.
Alisisitiza kuwa bandari hiyo itakuwa kitovu cha biashara ya kimataifa, hivyo kuchochea uchumi wa Taifa na kuongeza ajira kwa Watanzania.