Dar es Salaam. Wananchi wa visiwa vya Juma, Kasalazi, Ziragula na Bezi, vilivyoko ndani ya Ziwa Victoria mkoani Mwanza, wanatarajiwa kunufaika na huduma nafuu, na ya uhakika ya umeme kufuatia ushirikiano mpya wa mwaka mmoja uliotiwa saini kati ya kampuni tatu zilizojipanga kuboresha na kusambaza huduma hiyo.

Kampuni hizo ni PowerHut Renewables Limited ya Arusha na taasisi ya Assist International, Caterpillar Inc. ya Marekani pamoja na Mantrac Tanzania. Ubia huo unalenga kuboresha na kupanua miundombinu ya uzalishaji na usambazaji umeme ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka, hususan katika shughuli za uzalishaji mali.

Akizungumza kuhusu mpango huo, Mkurugenzi Mtendaji wa PowerHut, Dk Prosper Magali, amrsema hatua hiyo imekuja wakati muafaka ili kujibu matarajio ya wakazi wa visiwa hivyo wanaohitaji huduma bora za umeme.

“Matamanio ya watu ya kuboreshwa kwa huduma za umeme sasa yanashughulikiwa,” amesema.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Programu na Mikakati wa Assist International, Cheri Reynolds, amesema umeme wa uhakika huwapa watu fursa mpya za maendeleo katika elimu, afya na biashara.

“Umeme wa uhakika hujenga uwezekano mpya katika familia na jamii… Tumevutiwa kujiunga katika ushirikiano huu kuleta nishati inayojitegemea kusaidia elimu, huduma za afya na ukuaji wa uchumi,” amesema Reynolds.

Mpango huu unatekelezwa chini ya Caterpillar Electrification Initiative programu ya uhisani ya Caterpillar Inc inayolenga kusaidia upatikanaji wa huduma za umeme barani Afrika kwa kutumia teknolojia imara za kampuni hiyo, chini ya usimamizi wa Assist International.

Makamu wa Rais wa Caterpillar, Kitengo cha Umeme, Mellissa Busen, amese upatikanaji wa umeme nchini Tanzania ni suala nyeti linalohusiana moja kwa moja na ustawi wa jamii.

“Kupata umeme wa uhakika ni zaidi ya miundombinu, ni kuwezesha jamii, kuimarisha usalama na kufungua fursa,” amesema, akiongeza kuwa ushirikiano huo ni uthibitisho wa dhamira ya Caterpillar na Mantrac kuunga mkono maendeleo endelevu nchini.

Naye Meneja Usimamizi wa Biashara wa Mantrac Tanzania kwa Afrika Mashariki, Amr Zaki amesema kampuni hiyo inajivunia kushirikiana na wadau hao katika kusukuma mbele matumizi ya nishati endelevu.

“Tunafurahi kuleta suluhisho litakalobadilisha maisha na kuongeza uhimilivu wa jamii,” amesema.

Wanufaika wa Mradi

Kulingana na Dk Magali, mradi huo utawanufaisha wajasiriamali, hasa wa fani za useremala, uchomeleaji vyuma na wavuvi wanaohitaji huduma za kuchaji betri za boti, uhifadhi wa samaki kwenye majokofu na uzalishaji wa barafu.

Pia mpango huu utaleta mapinduzi katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wakazi wa visiwa hivyo, hatua inayolenga kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambavyo ni vigumu kupatikana visiwani na husababisha madhara ya kiafya na kimazingira.

“Huu ni ukombozi dhidi ya madhara ya moshi wa kuni na mkaa na kupunguza muda unaotumika kutafuta nishati hiyo badala ya kufanya shughuli za uzalishaji mali,” amesema.

Katika sekta ya afya, mradi utaboresha utoaji wa huduma katika zahanati, maduka ya dawa na maabara ndogondogo kwa kuwezesha upatikanaji wa mwanga wa uhakika, vifaa vya kuhifadhia dawa na chanjo, pamoja na mazingira bora kwa wajawazito kujifungua usiku.

Utekelezaji wa Mpango

Ubia huo ulianza rasmi Desemba 4, 2025, ambapo PowerHut itasimamia uzalishaji na uendeshaji wa miundombinu ya umeme katika visiwa hivyo, huku washirika wengine wakitoa fedha na teknolojia kwa maboresho yanayolengwa.

“Tunatarajia ushirikiano mkubwa kutoka serikalini, wizara husika na wadau wengine ili mpango huu utekelezwe ipasavyo na kuwanufaisha wananchi,” amesema Magali.

PowerHut kwa sasa inaendesha miradi minane ya umemejua kwa mfumo wa gridi ndogo, ikihudumia zaidi ya wakazi 2,000 katika visiwa vya Juma, Kasalazi, Ziragula, Bezi, Yozu, Chembaya, Sozia na Lyegoba.

Dk Magali amesema mahitaji ya nishati yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka, hivyo kuhitaji maboresho kupitia ushirikiano mpya ulioanzishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *