Haiti iko katika mgogoro wa kiusalama huku magenge mbalimbali yakipigania udhibiti wa maeneo katika mji mkuu na kwingineko huku yakiendelea kupanua shughuli zao za uhalifu.

Kutokuwepo kwa usalama kumesababisha mamia ya maelfu ya Wahaiti kuyahama makazi yao, jambo ambalo limeongeza mzigo katika migogoro ya kibinadamu na kiuchumi ambayo nchi hiyo inakabiliana nayo.

Kuna hofu kwamba magenge yanazidi kushirikiana na mitandao ya kimataifa ya uhalifu uliopangwa katika kusafirisha dawa za kulevya.

Washirika wa magenge wenye silaha wakitembea katika kitongoji cha Port-au-Prince

Umoja wa Mataifa

Ni dawa gani zimekamatwa na wapi?

Kilo 1,045 za kokeini, kiwango kilicoweka rekodi, zilikamatwa mwezi Julai 2025 karibu na eneo liitwalo Île de la Tortue, ambapo ni kisiwa kilicho kaskazini mwa Haiti, katika operesheni ya majini iliyofanywa na mamlaka za Haiti. Hii ilikuwa ni oparesheni kubwa zaidi ya kukamata dawa za kulevya nchini humo katika kipindi cha zaidi ya miaka 30.

Wiki mbili baadaye, kilo 426 za bangi zilitaifishwa huko Petite-Anse, karibu na Cap-Haïtien, ambako nako ni kaskazini mwa nchi hiyo.

Kumekuwa pia na ukamataji mwingine maeneo mengine. Wahaiti wawili walikamatwa Jamaica, pia mwezi Julai, wakiwa na zaidi ya kilo 1,350 za bangi.

Dawa hizi zilikuwa zinasafirishwa kwenda wapi?

Kokeini iliyokamatwa mwezi Julai inadaiwa ilitoka Amerika Kusini na ilikuwa inaelekea, kwa mujibu wa wachunguzi, kusambazwa katika maeneo ya Karibiani na Marekani.

Kuna pia ushahidi wa hivi karibuni uliopokelewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu UNODC unaonesha dawa hizo zinasafirishwa kwenda Ulaya.

Mwezi Agosti 2025, mamlaka za Ubelgiji zilikamata kilo 1,156 za kokeini katika bandari ya Antwerp kwenye kontena lililotokea Haiti.

Magenge ya Haiti yanahusikaje?

Magenge makubwa yamejikita katika njia muhimu zinazoingia na kutoka jijini Port-au-Prince pamoja na mipakani na Jamhuri ya Dominika, yakidhibiti njia kuu za usafirishaji wa dawa za kulevya pamoja na bidhaa nyingine haramu, ikiwemo silaha.

Udhibiti wa njia za ndani unayapa magenge uwezo wa kutoza wananchi kodi za lazima na pia kusafirisha dawa hizo bila kizuizi, nyingi zikielekezwa kusafirishwa nje.

Baadhi ya magenge yanaripotiwa kutoza ushuru kwenye boti na kujihusisha na uporaji wa kutumia silaha baharini, yakiongeza udhibiti wao kwenye biashara na njia za usafirishaji.

Taarifa kutoka JamaicAa pia zinaunganisha ukamataji wa silaha na biashara ya kubadilishana dawa za kulevya kwa silaha inayohusisha magenge ya Haiti.

Silaha na risasi mara nyingi husafirishwa kuingia Haiti kupitia njia zilezile zinazopitishwa dawa za kulevya.

© CPB/HSI

Kwa nini Haiti imekuwa eneo la kupitishia dawa za kulevya?

Shughuli nyingi za kimataifa za usafirishaji wa dawa za kulevya zimekuwa zikifanyika katika eneo la Île de la Tortue, eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa kitovu cha shughuli za uhalifu wa kimataifa kutokana na ukubwa wake na umbali wake.

Kihistoria lilitumiwa na maharamia na katika miongo ya hivi karibuni na mitandao ya uhalifu uliopangwa inayojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu na shughuli nyingine.

Mahali lilipo kijiografia, ambalo lina ufikiaji wa moja kwa moja kwa Bahamas na Jamaica, pamoja na Visiwa vya Turks na Caicos, linaufanya kuwa eneo zuri kwa ajili ya kuhifadhi na kupanga usafirishaji wa mizigo haramu.

Wafanyabiashara haramu wameweza kutumia changamoto za Haiti katika kujenga mfumo madhubuti wa sheria na magereza ambao ungeweza kukabiliana na ongezeko la magenge ya uhalifu na shughuli haramu wanazofanya.

Athari za kikanda ni zipi?

Haiti inageuka kwa haraka kuwa kitovu cha usafirishaji wa kimataifa wa dawa za kulevya. Wafanyabiashara waliokuwa wakihusika katika usafirishaji wa kokeini walikuwa raia wa Bahamas na Jamaica, jambo linaloonesha kuwepo kwa ushirikiano wa kikanda kati ya wahalifu hao na wale wa Haiti.

Ukamataji wa dawa za kulevya katika maji ya Haiti na Ulaya unaonesha njia za usafirishaji zilizo imara, zilizoratibiwa na zilizo na mtandao mpana, zinazo hitaji ushirikiano thabiti wa kikanda kutoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.

Njia mpya za usafirishaji dawa za kulevya pia zinaingiliana na usafirishaji wa watu kiharamu, ambapo raia wa Haiti wanahusishwa kwa kiasi kikubwa.

Wakati huohuo, biashara ya dawa za kulevya inachangia katika kuongezeka kwa machafuko ya kikanda, kudhoofisha utawala bora, kuvuruga uchumi na kuchochea vurugu.

Bandari, njia za biashara na sekta za utalii katika nchi zinazokumbwa na tatizo hili zinakabiliwa na changamoto kubwa za kiusalama na kuharibiwa kwa taswira ya nchi.

Walinzi wa Pwani wa Haiti wakiwarudisha wahamiaji waliokuwa wamekimbia nchi kupitia njia za usafirishaji haramu.

© US Coast Guard

UNODC inaisaidiaje Haiti kukabiliana na usafirishaji wa dawa za kulevya?

UNODC inaimarisha usalama wa mipaka, kuimarisha udhibiti wa baharini, kuendeleza uchunguzi unaotegemea taarifa za kiintelijensia na kushughulikia rushwa na uhalifu wa kifedha unaoruhusu mitandao ya usafirishaji kufanya kazi.

Kazi ya shirika hilo inaanzia mipakani, ambako Haiti inaendelea kuwa dhaifu zaidi kwa mtiririko wa bidhaa haramu.

Mpango wa kitaifa wa usimamizi wa mipaka uliobuniwa kuongeza uwezo wa kuzuia uingizaji wa bidhaa haramu katika bandari, viwanja vya ndege na mipaka ya nchi kavu, umeanzishwa kwa ombi la serikali ya Haiti.

Katika maeneo ya Baharini, Mpango wa Kimataifa wa UNODC wa Kukabiliana na Uhalifu wa Baharini unalenga kuimarisha Walinzi wa Pwani wa Haiti, ambao wana jukumu muhimu katika kulinda njia za baharini zinazotumika sana kusafirisha dawa za kulevya na usafirishaji haramu wa binadamu.

Nchi kavu, UNODC inaongeza uwezo wa vyombo vya sheria kufanya operesheni zinazotegemea intelijensia dhidi ya makundi ya uhalifu yaliyo katika usafirishaji haramu wa watu, biashara ya binadamu na shughuli nyingine zinazofanana. Kubadilishana taarifa kati ya Haiti na washirika wa kikanda, ambako ni muhimu katika kubaini na kuvunja mitandao ya uhalifu wa kuvuka mipaka, pia kumeimarishwa.

Kutambua kuwa usafirishaji wa dawa za kulevya kunawezeshwa na rushwa iliyokita mizizi na utakasishaji wa fedha chafu, UNODC inatekeleza mipango ya serikali inayolenga kuimarisha uadilifu wa taasisi na uwajibikaji.

Mahakama maalumu zimeanzishwa ambazo zina uwezo wa kushughulikia kesi za uhalifu wa kifedha, utakasishaji wa fedha, makosa ya magenge na masuala mengine nyeti ya jinai, kwa lengo la kupunguza ukwepaji wa sheria na kurejesha imani katika mfumo wa haki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *