Kutokana na kuendelea kwa changamoto ya uhaba wa maji katika kata ya Chanika Wilaya ya Handeni mjini, Mkoani Tanga, uongozi wa kata umeanza mikakati ya ndani ya kutatua kero hizo wakati wakiendelea kusubiri utekelezaji wa mradi mkubwa wa Miji 28 wenye thamani ya Sh bilioni 171.
Diwani wa kata hiyo, Habibu Mbota, amefanya ziara ya kutembelea vyanzo na vituo vyote vya maji katika kila mtaa wa Chanika ili kujionea hali halisi ya utoaji huduma, Ziara hiyo imebaini changamoto kadhaa ikiwemo baadhi ya vituo kushindwa kutoa huduma pamoja na wasimamizi wa vituo hivyo kutoweka wakiwa na fedha za makusanyo ya maji.
Changamoto hizo zimesababisha kudorora kwa huduma na kuibua lawama ambazo mara nyingi huishia kuelekezwa kwa viongozi wa juu, hali hiyo imemfanya Mbota kutoa msimamo mkali akisisitiza kuwa hawatakubali viongozi wa ngazi ya juu kulaumiwa kwa kero zinazoweza kutatuliwa katika ngazi za chini.
Ameziomba mamlaka ya maji HTM kuongeza ukali katika usimamizi na ukusanyaji wa mapato ili kuhakikisha huduma hazisimami na kwamba maji yanapatikana nyakati zote, hata kama ni kwa kiwango kidogo kilichopo.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata, Bahasha, ameomba kata kupatiwa mtaalamu wa masuala ya maji ili kupunguza mlundikano wa kero na kuongeza ufanisi katika kushughulikia matatizo ya wananchi.
#StarTvUpdate