Marekani. Kuna simulizi na tetesi nyingi zilizozungukia urafiki na uhusiano wa miaka mingi kati ya staa wa R&B, Toni Braxton, (58), na Birdman, (56), rapa na mkurugenzi wa Cash Money Records, lebo iliyomtoa Lil Wayne kimuziki.
Ukaribu wao ulianza pindi Birdman alipomshirikisha Braxton katika wimbo wake, Baby You Can Do It (2000) uliotayarishwa na Timbaland, na ulijumuishwa katika albamu yake ya kwanza iliyoitwa Birdman.
Toni Braxton, mkali wa kibao cha He Wasn’t Man Enough (2000), alitokea katika video hiyo ya Birdman kimahaba zaidi, ambapo walionekana wakikumbatiana na kucheza pamoja katika sehemu nyingi. Hata hivyo, ilichukua miaka kadhaa hadi kuja kuwa na uhusiano rasmi na hatimaye ndoa yenye utata, hivyo mlolongo huo wa mambo ndio uliochochea tetesi na uzushi mwingi kuhusu maisha yao kama ifuatavyo.
Kabla ya ukaribu na Birdman, Braxton alishafunga ndoa na mwanamuziki Keri Lewis ambaye uhusiano wao ulianza mwaka 1998. Na kufikia Desemba 2, 2001, wakajaliwa mtoto wa kwanza, Denim Cole Braxton Lewis.
Wakati akijiandaa kutoa albamu yake ya nne, More Than a Woman (2002), aligundua kuwa ana ujauzito wa mtoto wa pili. Ni ujauzito uliomsumbua sana kwani ulimlazimu kukaa kitandani kwa muda mrefu.
Mtoto wao wa pili, Diazel Ky Braxton Lewis alizaliwa Machi 31, 2003, na baadaye aligundulika ana autism (usonji), kitu ambacho kimemfanya Braxton kuwa mstari wa mbele kusaidia wanaopambana na ugonjwa huo.
Katika kitabu chake, Unbreak My Heart (2011), Braxton anadai huenda tukio la mtoto wake kupata autism ni “adhabu ya Mungu” kwa sababu katika ujana wake aliwahi kupata ujauzito na akautoa.
Braxton na Lewis walitangaza kuachana Novemba 2009, ila walitalikiana rasmi Julai 2013. Wakati hayo yote yakijiri tayari jina la Birdman lilikuwa likihusishwa na mwimbaji huyo aliyeibuka na kundi la The Braxtons.
Kwa mara ya kwanza tetesi za uwepo wa uhusiano wao ziliripotiwa na TMZ mnamo Mei 2016 baada ya Birdman kuhudhuria shoo ya Braxton kwenye tamasha la kwanza la Grammy Park.
“Mnajua kila mtu amekuwa akiniuliza kuhusu hili la Braxton na Birdman. Lakini swali ni, wako pamoja au wako kwenye uhusiano?” alisema mdogo wa Braxotn, Tamar kupitia ‘Insta story’ na kukoleza uvumi huo.
Wakati huo, Braxton hakuweka wazi wala kukataa tetesi za uhusiano huo, badala yake aliziongeza kwa kumwalika Birdman jukwaani wakati wa show yake katika ukumbi wa Fox Theater jijini Atlanta.
Katika video iliyopigwa na shabiki, Braxton alionekana akiimba jukwaani na band, na ghafla Birdman akajitokea mbele ya umati – wakasimama pamoja huku mashabiki wakishangilia na kuwaitwa ‘wanandoa’.
Kufikia Juni 2016, dunia ikazidi kuamini kuwa wawili hao wapo kwenye uhusiano rasmi baada ya kuonekana pamoja kwenye zulia jekundu katika hafla ya utolewaji wa tuzo za BET.
Walionekana wakiwa wamesogeleana sana huku wakivalia nguo nyeusi zilizofanana, na hii ilikuwa ni ishara kuwa urafiki wao wa kikazi umevuka mipaka fulani na kubeba sura nyingine tofauti na ile ya awali.
Hata hivyo, mtangazaji Wendy Williams alitoa maoni yake kuhusu picha zao katika hafla ya BET, akidokeza kuwa huwenda uhusiano wa Braxton na Birdman ulikuwa kiki ya kujitangaza tu kimuziki.
Lakini miezi michache baadaye, Birdman alimzawadia Braxton gari jipya aina Bentley SUV kwa ajili ya siku yake ya kuzaliwa akitimiza umri wa miaka 50. Mwaka uliofuatia, katika siku ya kuzaliwa ya Birdman ambapo alitimiza umri wa miaka 48, Braxton alimwimbia rapa huyo hadharani mbele ya mashabiki mjini New Orleans kisha akamkabidhi keki mbili na kumbusu.
“Kwa bahati nzuri kwangu, anapenda kufanya mambo yanayoonyesha ananijali,” Braxton alikiambia kipindi cha Braxton Family Values, akifafanua jinsi Birdman alivyo kwake.
“Yeye ni mwanaume mwenye ustaarabu wa ndani kwa ndani, na ananifanya nijisikie kupendwa,” alieleza mwimbaji huyo wa kibao maarufu, Long As I Live (2018).
Mnamo Januari 2018, Braxton alirudi na albamu yake ya tisa, Sex and Cigarettes (2018) lakini kabla ya albamu hiyo kutoka, wawili hao walitoa wimbo wao mwingine, Heart Away.
Albamu hiyo ilikuja mwezi mmoja baada ya Braxton kuthibitisha kuwa yeye na Birdman wamechumbiana kupitia trela ya msimu mpya wa kipindi cha familia yake, Braxton Family Values kilichoruka WeTV.
“Nina tangazo – nimechumbiwa,” Braxton aliwaambia dada zake kwa shangwe huku akionyesha pete ya almasi ya njano aliyovishwa na Birdman. Licha ya shangwe hizo, wawili hao walikuja kutengana Januari 2019, kisha miezi miwili baadaye wakadai bado wapo pamoja ila walikuja kuachana tena mwaka huohuo.
Hata hivyo, picha lao halikuishia hapo kwani miaka minne baadaye, Braxton na Birdman walikuja kufunga ndoa iliyoibua gumzo. Ndoa inayodaiwa kudumu kwa siku mbili tu.
Je, ni kwa namna gani?