
Dodoma. Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba amewataka viongozi wa umma kujiandaa kwenye sensa ya kila mtu kutaja mali zake na namna alivyozipata itakayofanyika kwa nchi nzima.
Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Desemba 11, 2025 wakati akizungumza na viongozi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ikiwa ni sehemu ya ziara zake kwa taasisi za Serikali.
Akizungumza kwenye mkutano na viongozi hao, amewataka watumishi wa umma kujiandaa kwa ajili ya sensa itakayofanyika nchi nzima, akisisitiza kuwa kila mmoja atapaswa kutaja mali alizonazo pamoja na kueleza kwa uwazi namna alivyozipata.
Kauli hiyo ya Dk Mwigulu imekuja siku chache baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete kusema yuko tayari kuhojiwa juu ya tuhuma zinazoelekezwa kwake mkitandaoni kuhusu umiliki wa mali, ikiwemo kuhusishwa na vituo vya mafuta vilivyofanyiwa uharibifu wakati wa maandamano Oktoba 29, 2025.
Kikwete aliwaeleza watumishi wa Sekretarieti hiyo kwamba ni vyema taarifa na malalamiko dhidi ya viongozi wa umma zikawa wazi na kuhojiwa kwa uwazi, ili wananchi wapate habari sahihi kuhusu kile kinachoendelea.
Kwa sababu hiyo, Kikwete aliwataka waandaaji wa uchunguzi wa maadili (Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma) kumuita bila hofu ili aeleze ukweli, na baada ya uchunguzi huo taarifa hiyo iwekwe wazi kwa umma na kwa waandishi wa habari.
Hata hivyo, leo Dk Mwigulu amewataka viongozi wote na watendaji kujiandaa kwa sensa ya kila mtu kutaja mali zake na namna alivyozipata.
“Mheshimiwa Waziri (Kikwete) nimeacha nchi itulie kwanza maana tumetoka kwenye sekeseke halafu nikianzisha lingine haitakuwa sawa, ila litakuja na mtaona sekeseke la watu,” haiwezekani watu wanakula keki za wengine,” amesema Dk Mwigulu.
Ameagiza watumishi wote sasa walazimishwe kujaza fomu za maadili na ziwe kwenye madaraja, zikianzia kwenye vitengo vyenye ushawishi mkubwa wa rushwa jambo alilosema lifanyike haraka kwa kushirikisha Taasisi ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa (Takukuru) na vyombo vingine.
Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, kuwa na mali nyingi siyo dhambi lakini dhambi inakuja namna mtu alivyopata mali hizo.
Kiongozi huyo amesema fomu za maadili zinajazwa na watu ambao hawahusiki zaidi kwenye rushwa ingawa wanaweza kuwa na ushawishi, akatolea mfano wa naibu mawaziri kwamba hawamo kwenye ushawishi wa moja kwa moja, lakini wanajaza fomu huku wajumbe wa kamati za tenda wanaandika matamko na kuweka tu kabatini.
Upigaji kwenye ukadiriaji
Akizungumzia suala la ukadiriaji amesema kuna baadhi ya watu wanaumizwa na maofisa wadogo ambao hawajazi hata fomu za maadili, badala yake wanajaza matamko na kuweka kabatini tu.
“Kuna watu wamefanya kazi miaka mingi kawatazameni walipostaafu hawana kitu, lakini kuna kakijana kalikuwa kaofisa furani hivi muda mfupi, kanakuwa na mali nyingi na wakati mwingine kijana wa form four (kidato cha nne) unamkuta anamiliki ghorofa, huyu kapata wapi,” amehoji Waziri Mkuu.
Ametolea mfano wa watu ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu zaidi kwenye utumishi wao, wakiwemo walimu, ambao hawana mwanya wa rushwa na wanaishi kwa mishahara midogo, lakini wanaweza kutenga muda wao wa ziada kuwafundisha watoto wa Kitanzania.
Wengine amewataja wauguzi, madaktari na vyombo vya ulinzi na usalama, kwamba hawalali usiku na mchana, ili kuhakikisha afya na maisha ya watu vinakuwa salama wakati wote, lakini keki ya nchi inawabagua.
“Naagiza kwa haraka iwezekanavyo kwa kushirikiana na vyombo vingine ikiwemo Takukuru ili wawaambie maeneo yote yenye viashiria vya rushwa, uandaliwe utaratibu wa kila mtumishi kujaza fomu za maadili na zifuatiliwe kujua kama wamedanganya au wamesema ukweli,” ameagiza Dk Mwigulu.
Katika kuimarisha maadili kwa watumishi wa umma nchini, Dk Mwigulu amesema ni muhimu kuanzishwa haraka mfumo utakaowezesha watumishi wote kujaza fomu za maadili.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa jambo hilo ufanyike kwa kasi, na kwamba fomu hizo zijazwe kwa uaminifu, uwazi na kwa kuzingatia madaraka ya kila mtumishi.
Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, daraja la kwanza ni wale wanaotoka kwenye vitengo vyenye ushawishi mkubwa wa rushwa hasa watu wa manunuzi, mikataba na wakadiriaji wa kodi; kisha lifuate daraja la watu wenye nafasi za ushawishi na baadaye daraja la watu wote.
Pia, Dk Mwigulu ametaja maeneo maeneo manne aliyoita ni tobo la uvujaji wa fedha za umma, kwamba manunuzi limekuwa la kwanza, likifuatiwa na ukadiriaji na makusanyo na kisha mikataba na utoaji wa leseni.
Amesema kuna taarifa za miradi mingi kukwama kwa sababu watu wanaohusika wanakuwa wamegawana fedha na kusababisha mkandarasi kusimamisha kazi, lakini kwenye utoaji wa leseni hasa za madini, wanyonge wanaporwa kupitia kwa maofisa.
“Nendeni mkachunguze, mtu anaomba leseni ya madini lakini kwa sababu ya uonyonge wake ikifika maeneo husika watu wanaona ni dili wanagawana na kumnyima mhusika haki yake na ndivyo inavyofanyika hata kwenye ardhi, haikubaliki,” ameonya.
Kauli ya wadau
Kauli ya Dk Mwigulu imeibua maoni tofauti ya wadao, ambapo Donald Kasongi, mkurugenzi wa taasisi ya Governance Link amesema kuwekwa kwa mfumo anaupendekeza, hakutasaidia kuwabadilisha viongozi wanaokiuka maadili, badala yake wafuate misingi ya utumishi wa umma, ambayo inafuatwa na dunia nzima katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
Kasongi ameeleza kuwa misingi hiyo inajumuisha kufanya kazi kama Serikali moja, tofauti na hali ilivyo sasa ambapo inaonekana kama kuna Serikali nyingi zinazotekeleza majukumu kwa mtindo usio pamoja.
Ameongeza kuwa watumishi wanapaswa kuishi kwa nidhamu katika maisha yao binafsi, kwani kwa sasa wengi wanaishi maisha yasiyoakisi maadili wala taratibu za utumishi wa umma.
Kwa upande wake mchambuzi wa masuala ya kisiasa Profesa Thabit Mponda, amesema mbali na agizo hilo, ni muhimu viongozi wa umma kuzingatia kiapo cha maadili ya utumishi wao kwa sababu wamepewa dhamana ya kusimamia rasilimali za Taifa, hivyo wasipozingatia kwa hiari yao hata watakiwe kujaza hizo fomu bado itakuwa ni kazi ya bure.
Profesa Mponda amesema vitendo vingi vya rushwa na kujilimbikizia mali vinafanywa na watumishi wa umma kwa sababu ndiyo wenye dhamana ya kusimamia miradi mingi ya maendeleo ambayo inagharimu fedha nyingi, hivyo kama hawatazingatia maadili hata kama sheria zitatungwa na kuwaunganisha wengine bado, watapokea rushwa na kujilimbikia mali.
Awali, kwenye mkutano huo, Waziri Kikwete amesema haiwezekani Tanzania kuwa na viongozi ambao wanalalamikiwa halafu watu wa maadili wako kimya.
Kikwete amesema kuna watu wanashutumiwa akiwemo yeye mwenyewe halafu hakuna mtu anayesimama kuwaita na kuwahoji ili kupata ukweli.
“Haiwezekani mtu akawa na meno, lakini Tume isipofanya kazi tutaendelea kuwa na viongozi wasiokuwa na uzalendo kwenye nchi hii, ni lazima tufanye kazi,” amesema.
Kamishina wa Maadili ya ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Sivangilwa Mwangesi amesema kwenye utendaji wao wanakwamishwa na kukosekana kwa ushahidi wanapowahoji watu kutaka ukweli, kwani wengi wanaogopa kujitokeza.
Jaji Mwangesi amesema uelewa wa kisheria kwa watu bado ni mdogo, ndiyo maana wanakosa taarifa sahihi za kufichua maovu.
Kamishina amesema katika mwaka wa fedha uliopita jumla ya mashauri 62 yalifikishwa mbele ya Sekretarieti ambapo asilimia 16 ya malalamiko hayo yalikuwa na dosari.