
Francesca Albanese, Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu amesema, Israel na Marekani pamoja na nchi zingine ambazo zilikuwa wasambazaji wakuu wa silaha kwa utawala huo, zinapaswa kugharimia ujenzi upya wa eneo la Ukanda wa Ghaza.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika jijini London, Uingereza kuhusu hali ya haki za binadamu katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, Albanese amebainisha kuwa inapaswa ifanyike tathmini kamili ya ushiriki uliofanywa katika mauaji ya kimbari ya Gaza, na kusisitiza kwamba si Israeli pekee bali mataifa yote yanayosaidia mauaji ya kimbari inapasa yakabiliwe na vikwazo.
“Lazima mataifa yavunje uhusiano na Israel, na lazima yaache kuifadhili kifedha na kuisaidia nchi inayoendeleza na ukaliaji haramu wa ardhi,” amesisitiza ripota huyo maalumu wa UN.
Akigusia suala la uwajibikaji, Albanese amesema, Israeli inapaswa ilipie gharama za ujenzi upya wa Ghaza, pamoja na Marekani, Ujerumani, na Italia, ambao ndio watoaji wakuu wa silaha.
Ameendelea kueleza kwamba, inapasa ufanyike uchunguzi mkali kuhusu ushiriki wa Uingereza katika mauaji hayo ya kimbari ya Ghaza kupitia utoaji huduma uliofanywa na serikali ya London kupitia vituo vyake vya kijeshi vilivyoko Cyprus.
Albanese amebainisha kwa kusema: “ikiwa Israel haitaki ishutumiwe kwa vitendo vya kikoloni, isionyeshe miamala kama ya dola la kikoloni, kama chombo cha kikoloni, ya kunyakua ardhi, na kuwahamisha watu”.
Huku akikumbusha kwamba miaka miwili ya mauaji ya kimbari ya huko Ghaza ni “mchanganyiko wa miaka 60 ya kutochukuliwa hatua (Israel),” Ripota maalumu wa UN wa masuala ya haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo wa kizayuni, amebainisha kuwa, hali hiyo haitasita “isipokuwa kama mambo yatabadilika huko London au Rome, au Berlin, au Paris”…/