
Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, ameishutumu Marekani kwa kutumia madai ya biashara haramu ya dawa za kulevya kama kisingizio cha kunyakua maliasili za nchi yake, hasa mafuta ya petroli.
Matamshi hayo ya Rais wa Venezuela yamekuja siku chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza kwamba nchi yake imetwaa meli kubwa ya mafuta ya Venezuela.
Akijibu matamshi ya Truump, Maduro ametangaza kuwa, “Barakoa imeanguka,” akisisitiza kwamba lengo halisi la hatua za Marekani ni mafuta ya Venezuela.
“Suala si biashara ya dawa za kulevya. Ni mafuta wanayotaka kuiba,” amesema Rais wa Venezuela, akiongeza kuwa dola la kibeberu linataka akiba ghafi, lami, na gesi ya Venezuela.
Ameihutubu Marekani moja kwa moja, akisema, “Mwizi, ondoka hapa.”
Maduro pia amesisitiza tena msimamo wa Venezuela wa kutetea mamlaka na maliasili zake, akisifu ustahimilivu wa watu wa Venezuela na akaapa kwamba nchi hiyo haitasalimu amri kamwe.
“Hapana kupigana vita kwa ajili ya mafuta. Hapana kumwaga damu kwa ajili ya mafuta,” amesema Nicolas Maduro.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais wa Colombia, Gustavo Petro aliiambia CNN kwamba kampeni ya Washington ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya Venezuela inaonekana kuchochewa na upatikanaji wa akiba kubwa ya mafuta nchini humo badala ya kile kinachodaiwa kuwa ni wasiwasi kuhusu “biashara ya dawa za kulevya.”