Sambamba na Israel kukiuka usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio jipya linaloitaka Tel Aviv kutekeleza uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuhusu eneo hilo la Palestina.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) Ijumaa tarehe 12 mwezi huu wa Disemba lilipasisha azimio ambalo limeitaka Israel iruhusu kufikishwa misaada ya kibinadamu katika eneo la Ukanda wa Gaza na kuwezesha usambazaji chakula, maji, dawa na mahema kwa wenyeji wa eneo hilo, kuheshimu kinga ya maeneo ya Umoja wa Mataifa na kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Azimio hilo limepasishwa kufuatia maoni ya ushauri yaliyotolewa hivi karibuni na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ambayo yameeleza wajibu wa Israel kama “utawala ghasibu” na pia kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Azimio hilo ambalo limewasilishwa na Norway na nchi nyingine zaidi ya 12, limepasishwa kwa kuungwa mkono na nchi 139. Nchi 12 zimelipinga na 19 hazikupiga kura. Kabla ya kupigwa kura kuhusu hali ya Wapalestina, Mwakilishi wa Kudumu wa Norway katika Umoja wa Mataifa, Merete Fjeld Brattested, alisema: “Mwaka 2024 ulikuwa moja kati ya miaka yenye ukatili mkubwa zaidi katika miongo mitatu iliyopita. Brattested aliongeza kuwa: “Mwaka wa 2025 unafuata njia hiyo hiyo, na kuna dalili chache kwamba mwenendo huu utapungua katika mwaka ujao (2026). Hali katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu inapaswa kupewa mazingatio.” Balozi wa Norway katika Umoja wa Mataifa aliongeza: “Raia wanalipa gharama kubwa zaidi. Heshima kwa kanuni za kibinadamu inapungua na kanuni za msingi zaidi za sheria za kibinadamu ziko chini ya shinikizo.”
Kwa upande wake, mwakilishi wa Marekani, Jeff Bartus alipinga azimio hilo kabla halijapigiwa kura, akitoa matamshi ya kuiunga mkono Israel na dhidi ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na maazimio yake. Akidai kwamba “azimio hilo la kumaonyesho litaibua mgawanyiko na kuzuia amani,” afisa huyo wa Marekani alisisitiza kwamba Washington intapiga kura dhidi ya azimio hilo na kutoa wito kwa nchi zingine kulipinga.
Hata hivyo, licha ya juhudi na kauli za mwakilishi wa Marekani, azimio hilo limepitishwa. Hii inaonyesha kupungua ushawishi wa Marekani duniani, na vilevile mshikamano wa nchi mbalimbali na watu wa Palestina wanaokandamizwa, ambao sasa wako chini ya mashinikizo zaidi kuliko hapo awali kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mnamo Disemba 5, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa wingi wa kura maazimio matano yanayoiunga mkono Palestina, ikiwa ni pamoja na kuongeza muda wa kazi za UNRWA, kulaani ujenzi wa vitongozi vya Wazayuni katika ardhi ya Palestina na kutetea haki za wakimbizi wa Kipalestina. Ingawa maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hayana dhamana ya utekelezaji, lakini yanaonyesha uungaji mkono wa jamii ya kimataifa kwa haki za wakimbizi wa Palestina na ongezeko la kutengwa Israel katika jukwaa la kimataifa.
Azimio la Ijumaa hii la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine limeonyesha kwamba jamii ya kimataifa ina msimamo mkali na muhimu dhidi ya mienendo ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu, hasa Ukanda wa Gaza. Azimio hilo, ambalo limepitishwa kwa uungwaji mkono mkubwa wa nchi wanachama, linaulazimisha utawala wa Israel kutekeleza uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuhusu utoaji wa misaada kwa watu wa Gaza na kuhakikisha watu wa eneo hilo wanapata chakula, maji, dawa, na makazi salama. Pia linasisitiza kwamba Tel Aviv haipaswi kuzuia shughuli za uokoaji na haipaswi kuwaweka raia wa Palestina katika hali ya ukimbizi na njaa.

Hatua hii ya Baraza Kuu inaweza kuonekana kama ishara ya kuongezeka mashinikizo ya kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Katika hali ya sasa ambapo, watu wa Gaza wanasumbuliwa na hali mbaya sana kutokana na sera za kikatili za Israel, licha ya makubaliano ya kidhahiri tu ya kusitisha mapigano, na kuna ripoti nyingi za uhaba mkubwa wa chakula na dawa, kupitishwa kwa azimio kama hilo kunaonyesha mshikamano wa kimataifa na watu wa Palestina. Kuungwa mkono azimio hilo na nchi 139 wanachama wa Umoja wa Mataifa pia kunaonyesha mwafaka mpana katika kulaani sera za utawala wa Kizayuni za uvamizi na vikwazo.
Azimio hilo pia ni muhimu sana kwa mtazamo wa kisiasa, kwa sababu Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kama taasisi jumuishi, linaakisi sauti ya wengi katika jamii ya kimataifa. Suala hili linaonyesha kwamba suala la Palestina bado ni kipaumbele katika ajenda ya kimataifa na kwamba jamii ya kimataifa haiko tayari kukaa kimya kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo hilo.
Kwa upande mwingine, azimio hilo linatuma ujumbe wa wazi kwa nchi zinazouunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel. Kuidhinishwa kwake na idadi kubwa ya nchi wanachama kumeonyesha kuwa sera za Tel Aviv zinazidi kutengwa katika nyanja za kimataifa, na hata baadhi ya washirika wa jadi wa utawala huo watalazimika kufikiria upya misimamo yao kutokana na mashinikizo ya maoni ya umma duniani.