Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania waweka akiba ya chakula walichonacho na waepuke matumizi yasiyofaa kutokana na hali ya kuchelewa kwa msimu wa mvua.

Waziri Mkuu amesema hayo leo Jumapili, Desemba 14, 2025, akizungumza na baadhi ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, ofisini kwake Mlimwa, Jijini Dodoma.

Amesema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),ilitoa utabiri wa mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli na mvua za msimu kwa kipindi cha Oktoba 2025 hadi Desemba 2025 pamoja na Novemba, 2025 hadi Aprili 2026 mtawalia.

“Kutokana na utabiri huo, baadhi ya mikoa nchini inatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha,” amesema.

“Pamoja na kuwa hakuna tishio la uhaba wa chakula kutokana na hifadhi ya chakula iliyopo nchini, lakini ni vema wananchi waendelee kuzingatia matumizi sahihi ya chakula. Tuna akiba ya chakula ya kutosha lakini ninawasihi wananchi waweke akiba na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima,” amesema.

Kwa upande wa wafugaji, Mwigulu amewataka kuweke mipango mizuri ya matumizi na uhifadhi wa maji na vyakula vya mifugo ili kukabiliana na hali hiyo.

Aidha, amewataka viongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) zihakikishe kuwa shehena za pembejeo zinahudumiwa kwa wakati ili usambazaji ufanyike kwa ufanisi.
#StarTvUpdate

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *