
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC Ali-Mohammad Naeini amesema kwamba ikiwa vita vitazuka, adui atakabiliwa na viwango vipya na vya hali ya juu vya nguvu ya kijeshi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Brigedia Jenerali Ali-Mohammad Naeini, Msemaji wa jeshi la IRGC la Iran amesema hayo katika mahijino na shirika la habari la Mehr na kueleza kwamba, Iran imefikia mafanikio mapya katika maeneo yote, ikiwa ni pamoja na silaha, mbinu, na mipango ya uendeshaji.
“Hakika tunatarajia kufikia mafanikio mapya katika nyanja zote; silaha, mbinu, na mipango. Hatufikirii vinginevyo,” Brigedia Jenerali Naeini amesisitiza.
Ameeleza bayana kwamba, iwapo vita vitaanza, adui bila shaka atakabiliwa na viwango vipya vya uwezo wa kijeshi wa Iran katika nyanja nyingi.
“Maendeleo haya lazima hatimaye yapatikane katika uwanja wa vita,” amesema Msemaji wa IRGC na kuongeza kwamba, adui atashuhudia athari za mabadiliko haya moja kwa moja iwapo vita vitatokea.
Naye Brigedia Jenerali Ali Jahanshahi, Kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, vikosi vya ulinzi vikiwa na zana kamili, silaha na uwezo viko tayari kukabiliana na tishio lolote la adui kwa kusikiliza amri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.