Majaji watatu wa serikali walimkuta Lai aliye na umri wa miaka 78, na hatia ya kuungana na wenzake wengine kushirkiana kinyume cha sheria kuhatarisha usalama wa China pamoja na kuchapisha taarifa za uchochezi. Hata hivyo Lai ambae ni mpinzani mkubwa wa serikali ya Beijing amekanusha mashitaka yote dhidi yake.
Lai, mmiliki wa gazeti la Apple Daily, lililofungiwa mwaka 2021, baada ya kuvamiwa na polisi na waandishi wengine wakuu kukamatwa, alitiwa nguvuni, mwezi Agosti mwaka 2020, chini ya sheria ya Beijing ya usalama wa taifa iliyowekwa baada ya maandamano makubwa ya kuipinga serikali mwaka 2019. Serikali ilifungia mali za gazeti hilo ambalo linasemekana kuukosoa utawala wake.
China ikiipongeza Hong Kong kwa kuadhibu kile ilichotaja kuwa “vitendo vya uhalifu vinavyohatarisha usalama wa taifa”.
Hadi sasa Lai amekuwa kizuizini kwa miaka mitano na muda mwingi amekuwa katika kifungo cha peke yake. Hali yake inasemekana kudhoofika na alionekana kukonda zaidi kuliko alivyokuwa. Jimmy Lai Pia amehukumiwa makosa mengine madogo kadhaa yanayohusiana na madai ya ulaghai na matendo yake ya mwaka 2019.
Kesi yake iliyoendeshwa bila ya jopo la majaji, imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu na Marekani, Uingereza, Ulaya na waangalizi wa kisiasa huku ikipima uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa mahakama katika koloni hilo la zamani la Uingereza lililorejea chini ya utawala wa China mwaka 1997.
Lai adaiwa kutumia mika mingi kupanga njama dhidi ya China
Mahakama imesema Lai alitumia miaka mingi kupanga njama dhidi ya Beijing. Akisoma hukumu yenye kurasa 855, Jaji Esther Toh alisema Lai alikuwa akitoa mwaliko wa mara kwa mara kwa Marekani ili kuiangusha serikali ya China, kwa kisingizio cha kuwasaidia wahongkong.
Mawakili wa Lai wamesema mteja wao hajawahi kuwa na nia kusambaratisha chama tawala cha kikomunisti.
Kati ya waliohudhuria kesi hiyo ni pamoja na mke wa Lai, mwanawe wa kiume na kadinali wa kikatoliki mjini Hongkong Joseph Zen. Hukumu itakayotolewa dhidi yake inaangaliwa kuwa jaribio la mahusiano kati ya China na Marekani.
Rais wa Marekani Donald Trump alisema alishazungumza kuhusu kesi ya Lai na China pamoja na Uingereza kupitia Waziri Mkuu wa taifa hilo Kier Starmer, ambaye alisema serikali yake imelifanya kuwa kipaumbele chake juhudi za kuhakikisha Lai ambae ni raia wa Uingereza anaachiwa huru.
Mwanawe wa kiume ameiomba Uingereza kuingilia kati na kumuokoa babayake. Kesi yake itaendelea tena Januari 12.
Mashirika ya kutetea haki za binaadamu yakiwemo Amnesty Internationa na shirika la kutetea waandishi habari la Reporters Without Borders wameikosoa hatua iliyochukuliwa na mahakama ya Beijing.