
Iran iko mbioni kukamilisha ujenzi wa kiwanda kikubwa cha nishati ya jua katika mkoa wa Isfahan wa katikati mwa Iran, mradi ambao unaotarajiwa kuzalisha umeme kwa karibu nyumba milioni 2.5 humu nchini.
Shirika la habari la Fars limeripoti kwamba kiwanda cha umeme cha Aftab Shargh kinatarajiwa kukamilika mwezi Machi 2027, kikiwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa jumla wa megawati 600 (MW).
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwanda hicho cha umeme, kilichoko katika eneo la mashariki mwa Kuhpayeh la Isfahan, tayari kinaingiza megawati 120 za umeme kwenye gridi ya taifa ya Iran baada ya awamu ya kwanza ya mradi huo kuanza kutumika mwezi Julai mwaka huu.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, kituo hicho kitapunguza uzalishaji wa COâ‚‚ kwa takriban tani milioni moja kila mwaka nchini Iran, ikibainisha kuwa uzalishaji wake wa umeme utatosha kukidhi mahitaji ya umeme ya karibu watu milioni 10 au takriban familia milioni 2.5.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Kampuni ya Chuma ya Mobarakeh ya Iran ambayo ni mzalishaji mkubwa zaidi wa chuma katika ukanda wa Asia Magharibi, imeajiri zaidi ya wafanyakazi 3,000 katika ujenzi na ufanikishaji wa mradi wa Aftab Shargh maneno ambayo yana maana ya “Mwanga wa Jua wa Mashariki” kwa lugha ya Kifarsi.
Kampuni hiyo inahusika katika miradi kadhaa ya nishati huko Isfahan, ambao ni moja ya mikoa yenye viwanda vingi zaidi nchini Iran. Kampuni hiyo ni mchangiaji muhimu katika mpango wa Iran nchi wa kupanua uwezo wa uzalishaji wa umeme mbadala wa MW 30,000 katika kipindi cha miaka minne ijayo.
Kwa sasa Isfahan inamiliki MW 240 za mashamba ya nishati ya jua na imekusudia kuwa na zaidi ya MW 470 ifikapo mwezi Februari mwakani.