
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema zaidi ya Wapalestina 1,000 wamepoteza maisha katika Ukanda wa Gaza kati ya Julai 2024 na Novemba 2025, wakisubiri ruhusa ya utawala wa Israel kuhamishwa kwa ajili ya matibabu kutoka kwa mamlaka za Kizayuni.
Kwa mujibu wa Rik Peeperkorn, mwakilishi wa WHO katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, jumla ya wagonjwa 1,092 walifariki katika kipindi hicho, idadi ambayo inadaiwa huenda ikawa imepunguzwa kwa sababu inategemea vifo vilivyoripotiwa pekee.
Peeperkorn alieleza kuwa WHO imezitaka nchi zaidi kukubali wagonjwa kutoka Gaza na kuruhusu operesheni za uhamishaji wa matibabu kuendelea hadi Ukingo wa Magharibi, ikiwemo Mashariki mwa al-Quds. Aliongeza kuwa kati ya hospitali 36 zilizopo Gaza, 18 pekee ndizo zilizoendelea kutoa huduma kwa kiwango cha chini, huku asilimia 43 ya vituo vya afya vya msingi vikiwa vimeathirika. Aidha, kulikuwa na upungufu mkubwa wa dawa muhimu na vifaa vya matibabu, hususan vinavyohitajika kwa wagonjwa wa magonjwa ya moyo.
Licha ya ongezeko la idhini kwa baadhi ya vifaa vya matibabu kuingia Gaza, Peeperkorn alisema mchakato wa kupeleka dawa na vifaa vya hospitali bado ni wa taratibu na mgumu bila sababu. WHO imeendelea kukumbana na changamoto za kuingiza vitendanishi vya maabara na vipuri muhimu vya mashine, ambavyo mara nyingi hukataliwa kuingia kwa kisingizio cha kutumika kwa matumizi mawili. Alisisitiza kuwa utawala wa Kizayuini wa Israel unapaswa kutoa idhini ya jumla kwa vifaa vya matibabu ili kukidhi mahitaji ya dharura.
Zaidi ya hayo, Peeperkorn alibainisha kuwa Kimbunga Byron kilipiga Gaza kwa nguvu, na kuongeza mateso ya familia zilizokwisha kufurushwa. Alionya kuwa hali ya baridi kali, ikichanganyika na ukosefu wa maji safi na huduma za usafi, inaweza kusababisha ongezeko la maambukizi ya mapafu, homa ya ini na magonjwa ya kuhara. Watoto, wazee na wagonjwa wa magonjwa sugu wapo katika hatari kubwa zaidi.
Tangu kusitishwa kwa mapigano Oktoba 10, jeshi katili la Israel limevunja makubaliano mara kadhaa, na kusababisha vifo vya angalau Wapalestina 386 na kujeruhi wengine 1,018. Tangu utawala haramu wa Israel uanzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, jeshi lake katili limeua zaidi ya Wapalestina 70,300, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi zaidi ya 171,000.