Orodha hiyo inaangazia nchi 20 zilizo katika hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na migogoro mipya ya kibinadamu au kuzorota kwa hali ya dharura ya kibinadamu mwaka 2026.
Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Sudan kuongoza orodha hiyo, iliyochapishwa leo Jumanne.
Mkurugenzi Mtendaji wa IRC, David Miliband, amesema katika taarifa kwamba,na hapa ninanukuu “Kile ambacho IRC inaona katika maeneo husika si jambo la bahati mbaya. Orodha ya Uangalizi ya mwaka huu ni ushahidi wa mateso lakini pia ni onyo kwamba bila hatua za haraka kutoka kwa wale wenye uwezo wa kuleta mabadiliko, mwaka 2026 unaweza kuwa mwaka hatari zaidi kuwahi kushuhudiwa.”
Kulingana na orodha hiyo, baada ya Sudan kunafuata Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi—maeneo ya Wapalestina ambayo IRC huyachukulia kwa pamoja—kisha Sudan Kusini, Ethiopia na Haiti.
IRC ilisema kuwa ingawa nchi hizi zinahifadhi takribani asilimia 12 tu ya idadi ya watu duniani, zinachangia asilimia 89 ya watu wote wanaohitaji msaada wa kibinadamu. Pia iliongeza kuwa inakadiriwa nchi hizo zitakuwa na zaidi ya nusu ya watu maskini kupindukia duniani kufikia mwaka 2029.
Umoja wa Mataifa pia umeelezea mgogoro wa Sudan, kama mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani. Kizungumzia majanga haya, huyu hapa Filippo Grandi, Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusu Masuala ya Wakimbizi (UNHCR). Mwaka uliopita ulishuhudia misukosuko mfululizo, dhoruba moja baada ya nyingine. Kwa ujumla, imekuwa dhoruba kamili kabisa. Tunashuhudia ukatili usioisha unaotekelezwa nchini Sudan, Ukraine, Gaza na Myanmar.”
Vita vilizuka nchini Sudan mwezi Aprili 2023 kufuatia mvutano wa madaraka kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces, kabla ya mpango wa mpito kuelekea utawala wa kiraia, na kusababisha mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani.
Zaidi ya watu milioni 12 tayari wameyakimbia makazi yao kutokana na vita vinavyoendelea nchini Sudan, ambapo wahudumu wa misaada wanakabiliwa na ukosefu wa rasilimali za kuwasaidia wanaokimbia, wengi wao wakiwa wamebakwa, kuporwa au kupoteza wapendwa wao kutokana na ghasia hizo.
Katika ripoti hiyo yenye kichwa “New World Disorder”, IRC inasema mamilioni ya watu nchini Sudan wanakabiliwa na ukatili uliokithiri, njaa na magonjwa. Nchi nyingine zilizoko kwenye orodha hiyo ni Myanmar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mali, Burkina Faso, Lebanon, Afghanistan, Cameroon, Chad, Colombia, Niger, Nigeria, Somalia, Syria, Ukraine na Yemen.
