
Iran imelaani rasmi vitisho “vikubwa na vya wazi” vya vita vya Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu uwezo woa kiulinzi na miraidi ya nyuklia ya nchi hii inayotekelezwa mwa malengo ya amani na kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani vitisho hivyo.
Trump alitoa vitisho hivi dhidi ya Iran siku ya Jumatatu katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Trump alitishia mbele ya waandishi wa habari kwamba ataangamiza makombora ya Iran iwapo Tehran itajaribu kujizatiti tena katika uwanja huo.
“Sasa nasikikia kwamba Iran inajaribu kujijenga tena, na kama ndivyo, tutawaangusha,” alidai Trump katika mkutano na waandishi wa habari.
Trump pia alidai kuwa ataunga mkono shambulio la Israel dhidi ya Iran iwapo Iran itaendelea na mpango wake wa makombora ya balistiki na silaha za nyuklia.
Amir Saeid Iravani Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema katika barua aliyowatumia Katibu Mkuu wa umoja huo Antonio Guterres na kwa Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Samuel Zbogar kwamba matamshi ya Trump ni sawa na “vitisho vikali na vya wazi vya utumiaji mabavu Rais wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran”, na ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Balozi Iravani amelitaka Baraza la Usalama la UN kulaani vikali vitisho vya wazi vya Rais wa Marekani kuhusu kutumia nguvu dhidi ya Iran suala ambalo ni ukiukaji mkubwa wa mkataba wa Umoja wa Mataifa
Amir Saeid Iravani amebainisha kuwa: Kauli hizi za uchochezi na za kushadidisha kutishia matumizi ya nguvu, zinazoelekezwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, hususan Ibara ya 2(4), ambayo inakataza bila shaka matumizi na kutoa vitisho vya utumiaji mabavu dhidi ya mamlaka ya kujitawala au uhuru wa kisiasa wa nchi yoyote.