Dar es Salaam. Wakati Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) likiendelea na usajili wa Ma-DJ na washereheshaji (Ma-MC), kumeibuka madai ya kutokuwapo usawa wa ada za vibali zinazotozwa.

Hivi karibuni Basata iliwataka Ma-DJ na Ma-MC kuzingatia takwa la kikanuni kwa kuhakikisha kila mmoja anakuwa na kibali hai hadi kufikia Januari 31, 2026, ambacho kitawapa uhalali wa kufanya shughuli za sanaa.

Taarifa iliyotolewa na Basata ilieleza watakaokwenda kinyume cha utaratibu huo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Akizungumza na Mwananchi Desemba 31, 2025, Ofisa Sanaa katika dawati la usajili la Basata, Gabriel Awe amesema baadhi yao wameanza kujisajili na wanatarajia hadi Januari 31, 2026 wote watakuwa wametimiza takwa hilo la kikanuni.

Amesema ada ya usajili ni Sh10,000 na ada ya kibali ni Sh40,000, hivyo atakayekiuka atachukuliwa hatua ikiwamo kutozwa faini ya papo kwa hapo.

Kanuni hiyo imepokewa kwa mitazamo tofauti na Ma-DJ wanaodai gharama hiyo ni kubwa kulinganisha na inayotozwa kwa kada nyingine, ikiwamo wasanii wa Bongo Fleva.

Katibu Mkuu Taifa wa Chama cha Ma-DJ wenye taaluma (TPDA), Asanterabbi Mtaki, amesema kama Basata ilitaka kuweka usawa, basi wasanii wote wangelipa kiwango kimoja.

“Ma-DJ na Ma-MC tunatakiwa kulipa ada ya usajili Sh10,000 na ada ya kibali Sh40,000, wakati wasanii wengine, wakiwamo wanamuziki wao walipa ada ya usajili Sh10,000 na ada ya kibali Sh10,000, kwa nini sisi iwe zaidi?” amehoji.

Amesema siyo kwamba hawataki kujisajili na kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni za Basata, bali kiwango cha ada walichowekewa ni kikubwa kulinganisha na vipato wanavyoingiza.

“DJ akienda kupiga sehemu pesa kubwa atakayolipwa ni Sh50,000, ingawa wapo wanaolipwa hadi Sh25,000 na wengine Sh10,000. Japo wapo Ma-DJ wachache na wanahesabika, anaweza kupiga kazi moja akalipwa hadi Sh2 milioni,” amesema na kuongeza:

“Kwa DJ kama huyo ana familia, amepanga na ana mahitaji mengine unataka tena alipie Sh50,000 Basata si sawa.”

Amesema Basata inapaswa kuweka usawa kwa wasanii wote, siyo wengine watozwe ada ya vibali Sh10,000 na wengine Sh40,000.

Kwa upande wa washereheshaji, baadhi wamesema utaratibu huo ni mzuri na upo kwa muda mrefu.

MC Makena Bryceson, amesema kuendesha shughuli hizo bila kibali cha Basata ni ubangaizaji, akibainisha hiyo ni taaluma kama zilivyo nyingine.

“Kuwa na kibali cha kuendesha shughuli za sanaa ni kujirasimisha kisheria, unakuwa hai na kupata faida nyingi, ikiwamo kukubalika na kutambuliwa kisheria na hata kupata fursa nyingine kama vile za mikopo kwenye mfuko wa utamaduni,” amesema.

Ameshauri elimu kuhusu faida za kuwa na vibali itolewe kuanzia ngazi ya kijiji maana wengi hawazijui, akieleza gharama ya Sh50,000 ni ya kawaida.

Kwa upande wake, MC Mcpeter_events amesema utaratibu wa Basata ni mzuri kwani unasaidia kuwaweka washereheshaji katika namna maalumu ya kutambulika rasmi kama kada inayochangia vijana wengi kujiajiri.

“Utaratibu huu ni katika jitihada ya kuturasimisha na kutuwekea utambuzi rasmi katika jamii,” amesema.

Ufafanuzi wa Basata

Akizungumzia tofauti ya viwango vinavyotozwa, Awe amesema vimetokana na maoni ya wadau wenyewe wa tasnia ya sanaa.

“Wakati tunaandaa kanuni mwaka 2018 tulizunguka nchi nzima kupata maoni, maofisa utamaduni waliwakusanya wadau wa sanaa, tukachukua maoni yao na kutengeneza kanuni ambazo tulizipeleka Hazina na kisha kupitishwa na Bunge,” amesema na kuongeza:

“Tatizo wakati tunawaambia watoe maoni wengine hawatilii maanani, jambo likishapitishwa ndipo malalamiko yanaibuka, ndicho kinatokea kwa Ma-DJ.”

Hata hivyo, Awe amesema kiwango cha Sh50,000 kimepunguzwa kwani kilichopelekwa Hazina awali kilikuwa Sh90,000.

“Kabla ya kupitishwa kanuni za 2018 ilikuwa ni Sh40,000 kwa wasanii binafsi wote, tulikusanya maoni kwa wadau wote ili kufanya maboresho, kwenye maoni wasanii wengine wakataka ipunguzwe iwe Sh20,000 ambayo ni ada Sh10,000 na usajili Sh10,000,” amesema.

Ameeleza: “Ma-MC wao wakasema hawataki kufananishwa na wasanii, hadhi yao ni kubwa wakataka walipe Sh200,000, tulipeleka maoni hayo Hazina na kiwango kilichorudi kutoka Hazina kikawa cha Sh10,000 ya usajili na ada Sh40,000.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *