
Zaidi ya watu 40 waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya Venezuela siku ya Jumamosi, wakiwemo raia na wanajeshi, gazeti la New York Times limeripoti, likimnukuu afisa mkuu wa Venezuela ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Gazeti hilo limesema kuwa limefanyia uhakiki kanda za video zinazoonyesha moshi mzito na miripuko ya mara kwa mara karibu na Uwanja wa ndege wa La Carlota katika mji mkuu wa Venezuela wa Caracas.
Huko Catia La Mar, mji ulio magharibi mwa mji mkuu, Caracas, shambulio la anga lilipiga jengo la ghorofa tatu la kiraia, na kuporomosha kuta zake, lilisema gazeti hilo, likibaini kuwa ajuza mmoja aliuawa, na mtu mwingine kujeruhiwa vibaya.
Vyombo vingi vya habari vya Marekani, vikinukuu vyanzo vya serikali ya Venezuela, viliripoti kwamba pamoja na Caracas, shabaha za kijeshi katika majimbo ya pwani ya Caribbean ya Miranda, Aragua, na La Guaira pia yalishambuliwa.
Nchi mbalimbali duniani zimeendelea kulaani vikali mashambulizi hayo ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela. Nchi hizo zimeeleza wasiwasi wao kuhusu uhalali, maadili na taathira hatari za uvamizi wa Marekani huko Venezuela.
Afrika Kusini jana Jumamosi ilionyesha wasiwasi wake mkubwa juu ya “uvamizi wa kijeshi” uliofanywa na Marekani dhidi ya Venezuela, pamoja na kutekwa nyara kwa Rais Nicolas Maduro na mkewe.
“Vitendo vya Marekani vinajumuisha ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambao unazitaka nchi zote wanachama kujiepusha na tishio au matumizi ya nguvu dhidi ya uadilifu wa eneo au uhuru wa kisiasa wa nchi yoyote,” Wizara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano ya Afrika Kusini imesema katika taarifa.
Hali kadhalika Afrika Kusini imetoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha mkutano wa dharura wa kujadili kadhia hiyo ya Venezuela.