
Serikali ya Uhispania imeelezea wasiwasi mkubwa ilionao kuhusiana na hali mbaya ya Gaza na muendelezo wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania ameonyesha wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kutoa wito wa kusimamishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii X, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania José Manuel Álvarez alielezea uungaji mkono kwake kikamilifu kwa amani ya kudumu Gaza na kukomeshwa kwa vurugu katika Ukingo wa Magharibi. Aliandika: “Hali ya kibinadamu huko Gaza ni mbaya sana. Vikwazo vinavyokabili mashirika ya kibinadamu havikubaliki na vinazidisha hali hiyo.”
Aidha amebainisha kuwa, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA na asasi zingine zenye mfungamano na Umoja wa Mataifa lazima yaweze kufanya kazi kwa uhuru huko Gaza na Ukingo wa Magharibi. Tutashiriki katika ujenzi mpya ili watu wa ukanda huo wawe na mustakabali katika ardhi yao wenyewe.
Wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alilaani marekebisho ya sheria yaliyopitishwa na Bunge la utawala wa kizayuni wa Israel, Knesset Desemba 29, yanayohusu kusitishwa shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), pamoja na mashirika mengine 30. Katibu Mkuu wa UN amesema, marekebisho hayo yanalenga kuzidisha kuzuia uwezo wa UNRWA kufanya kazi na kutekeleza majukumu yake yaliyoidhinishwa.