Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imeitaka jamii ya kimataifa kuheshimu uhuru na mamlaka ya kitaifa ya Venezuela kufuatia mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya nchi hiyo yaliyopelekea kukamatwa Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro na mkewe.

ECOWAS jana Jumapili ilisema katika taarifa yake kwamba inafuatilia kwa wasiwasi matukio yanayojiri Venezuela. 

Huku ikitambua haki ya nchi mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na ugaidi na biashara haramu ya dawa za kulevya, Jumuiya ya ECOWAS imesema kuwa inapenda kuikumbusha jamii ya kimataifa wajibu wake wa kuheshimu uhuru na mamlaka ya kitaifa ya kila nchi kama ilivyoainishwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa, hasa kifungu cha 2 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

ECOWAS pia imetangaza kuwa bega kwa bega na uungaji mkono wake kwa wananchi wa Venezuela katika juhudi zao za kuandaa mustakabali wa nchi yao kupitia mchakato jumuishi.

Gazeti la New York Times jana liliripoti kuwa, watu 80 wameuawa katika mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela juzi Jumamosi. New York Times limemnukuu afisa wa ngazi ya juu wa Venezuela na kuripoti kuwa idadi ya watu waliouawa huwenda ikaongezeka. 

Vladimir Padrino Waziri wa Ulinzi wa Venezuela jana alisema kuwa aghalabu ya walinzi wa Rais Maduro wameuawa katika oparesheni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Caracas. 

Rais wa Venezuela na mkewe waliwasili New York Jumamosi jioni na sasa wanashikiliwa katika Kituo cha Magereza cha Metropolitan huko Brooklyn. Wanakabiliwa na mashtaka ya biashara haramu ya dawa za kulevya na wanadaiwa kushirikiana na magenge yaliyotajwa kama taasisi za kigaidi. Maduro amekanusha tuhuma hizo na maafisa nchini Venezuela wametaka achiliwe huru mara moja yeye na mkewe. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *