Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel zinaendesha “vita laini” ili kuvuruga uthabiti na utulivu nchini likiwa ni jaribio la kufidia kushindwa kwao katika vita vya siku 12 vya mwezi Juni zilivyoanzisha dhidi ya Iran.

Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi ameyasema hayo Jumapili katika mkutano na makamanda wa polisi na maafisa wengine wa jeshi hilo sambamba na maandamano ya hapa na pale yanayoshuhudiwa katika miji ya Iran kulalamikia hali ngumu wa uchumi.

Amesema taifa la Iran litategemea utambulisho wake wa Kiiran na Kiislamu na maumbile yake ya kupenda amani na kuonyesha Muqawama dhidi ya maadui, na halitawaruhusu kamwe wazusha machafuko na wale waliohadaiwa na maadui kufanya vitendo vya kiadui dhidi ya nchi.

“Maadui, na hasa Marekani na utawala wa Israel, wanalenga kuchochea mvurugiko wa usalama nchini Iran kwa kutumia zana za vita laini ili kufidia kushindwa kwao katika vita vya kulazimisha vya siku 12”, amebainisha Jenerali Mousavi.

Baada ya Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel kushindwa waziwazi na kukatishwa tamaa na uchokozi wao ambao haukuzaa na matunda, waligeukia vita laini na mashinikizo ya kiuchumi ili kujaribu “kusababisha mvurugiko wa usalama na machafuko nchini kama njia ya kufidia kushindwa kwao,” amefafanua Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran.

Mousavi amebainisha kuwa wafanyabiashara na wenyemaduka walitoa madai yao halali na ya haki ya kutaka kuwepo na uthabiti wa kiwango cha upandaji na ushukaji wa thamani ya sarafu ya taifa kulinganisha na sarafu za kigeni na kuboreshwa hali ya biashara.

Hata hivyo, amesema, Marekani na utawala wa Israel zilituma “kwa haraka na kwa namna ya kushangaza” maajenti wao waliopewa mafunzo wayatumie vibaya maandamano hayo ili kuvuruga usalama wa taifa na amani kupitia operesheni za kisaikolojia na mbinu za vita vya utambuzi.

Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran amewasifu wananchi wenye basira na uelewa wa Iran kwa kujitenga haraka na wafanyafujo na wale wanaotaka kuzusha machafuko…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *