Rais wa Marekani kwa mara nyingine tena amekariri kauli zake za uingiliaji kati dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatia matukio ya hivi karibuni hapa nchini.
Katika hali ambayo, maafisa wa Iran wanasisitiza kusikilizwa sauti za waandamanaji na kushughulikiwa matakwa yao, Donald Trump, akizungumza na waandishi wa habari kwenye ndege ya rais siku ya Jumapili, aliionya tena Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji. Katika siku za hivi karibuni, maandamano yamefanyika nchini Iran kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa hasa kupanda kwa sarafu ya dola na kulegalega hali ya kiuchumi.
Matamshi ya Donald Trump ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran yanatolewa wakati ambapo maafisa katika Jamhuri ya Kiislamu, akiwemo Rais Masoud Pezeshkian, wamesema kwamba kuwaheshimu watu na kusikiliza madai yao ni msingi wa utawala.
Hapo awali Trump alikuwa amechapisha chapisho kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii kuhusu kuwaunga mkono waandamanaji wa Iran. Katika siku za hivi karibuni, Rais wa Marekani pia ameitishia Tehran kwa shambulio la kijeshi kwa kisingizio cha juhudi zake za kujenga upya vituo vyake vya nyuklia na kuimarisha uwezo wake wa makombora kufuatia vita vya siku 12, na pia kwa kisingizio cha kuwaunga mkono waandamanaji nchini Iran.
Akijibu madai na vitisho vya Rais wa Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyyed Abbas Araqchi alielezea matamshi ya Trump kama “yasiyo na busara na hatari” na akasema misimamo hii huenda iliathiriwa na mikondo inayopinga diplomasia au inayoona kuwa si lazima. Aliongeza: “Taifa kubwa la Iran, kama ilivyokuwa hapo awali, litakataa kwa dhati kuingiliwa mambo yake ya ndani. Vile vile, vikosi vyetu vyenye nguvu viko macho na vinajua haswa wapi pa kulenga iwapo kutatokea ukiukaji wa uhuru na mamlaka ya kujitawala Iran.”

Madai ya hivi karibuni ya Trump ya kile kinachoitwa uungaji mkono kwa watu wa Iran yanatolewa wakati ambapo ameweka vikwazo na mashinikizo makubwa zaidi kwa Iran kwa kupitisha sera ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa baada ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei 2018, na wakati wa muhula wake wa pili kama rais, pia ameanzisha kampeni ya mashinikizo ya kiwango cha juuu kabisa dhidi ya Iran, akiunga mkono moja kwa moja utawala wa Kizayuni katika kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran wakati wa vita vya siku 12. Inaonekana kwamba lengo kuu la Trump katika kauli zake za hivi karibuni zinazotishia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuchochea machafuko na kuhimiza maandamano yanayoendelea na vitendo vya vurugu na uharibifu.
Wakati huo huo, kauli za hivi karibuni za Rais wa Marekani kuhusu huruma na kuwajali wananchi wa Iran haziwezi kuchunguzwa pasi na kuzingatia na historia ya tabia yake na sera zake kuhusu Iran. Wakati mtu ambaye ametumia shinikizo la kiuchumi, kisiasa na hata vitisho vya kijeshi mara kwa mara dhidi ya taifa wakati wa muhula wake wa uongozi anapodai leo kwamba, anawaonea huruma na kuwajali wananchi wa Iran, madai haya ni kama utata wa wazi kuliko msimamo wa uaminifu. Ukosoaji wa dai hili unahitaji mapitio ya rekodi ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa” dhidi ya Iran. Sera hii ilijumuisha vikwazo vya kiuchumi jumuishi ambavyo havikulenga serikali ya Iran pekee bali pia maisha ya kila siku ya watu. Vikwazo hivyo vilisababisha kushuka kwa kasi kwa thamani ya sarafu ya taifa, upatikanaji mdogo wa dawa na bidhaa za kimsingi, na kuongezeka kwa ugumu wa maisha kwa mamilioni ya Wairani. Tunawezaje kukubali kwamba mtu aliyebuni na kutekeleza sera kama hiyo sasa anaweza kujionyesha kama mwenye huruma kwa watu wa Iran? Hapana shaka kuwa, huruma ya kweli haiendani na kuwashinikiza na kuwanyima watu mahitaji yao ya kimsingi ya maisha.
Kwa upande mwingine, Trump amekuwa pamoa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika sera zake za kigeni. Hatua yake ya kuunga mkono bila masharti vitendo na uhalifu wa Israel katika eneo, ikiwa ni pamoja na vitisho na mashambulizi dhidi ya Iran, kunaonyesha kwamba, wasiwasi wake mkuu haukuwa watu wa Iran bali maslahi ya washirika wa kikanda wa Marekani. Kujiunga na Israel katika kuishinikiza Iran, hasa katika uwanja wa kijeshi, kumetishia usalama na amani ya watu wa Iran. Kwa hivyo, madai yake ya kuwajali watu wa Iran ni kama propaganda na wenzo wa kisiasa kuliko simulizi halisi ilivyo.

Matamshi ya uingiliaji kati ya Trump pia yanaonyesha mtazamo wake usio wa kweli kuhusu watu wa Iran. Amejaribu mara kwa mara kuleta mgawanyiko kati ya watu wa Iran na serikali katika hotuba zake, na hivyo kuhalalisha sera zake. Kwa msingi huo, aina ya kauli kama hizi hazitolewi kwa huruma, bali ni kuendeleza malengo ya kisiasa na kijiopolitiki ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi. Huruma ya kweli inahitaji heshima kwa uhuru, mamlaka na haki ya kujitawala kwa mataifa, na si kuingilia mambo yao ya ndani ya mataifa mengine.
Jambo lingine muhimu ni kwamba Trump ametumia lugha ya vitisho katika matukio mengi. Tishio la shambulio la kijeshi au kuongeza vikwazo hakuwezi kamwe kuwa ishara ya huruma. Mbinu kama hiyo inaweka shinikizo la kisaikolojia na kiuchumi kwa watu na kuunda mazingira ya kutokuwa na utulivu katika nchi. Kama angekuwa na wasiwasi wa kweli kuhusu watu wa Iran, basi angepaswa kuchagua njia ya mazungumzo na ushirikishwaji wenye kujenga badala ya vitisho na vikwazo.
Kwa ujumla, madai ya Trump ya kuwaonea huruma watu wa Iran ni tofauti kabisa na rekodi yake. Sera zake za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa, uungaji mkono wake kwa Israel katika kutishia Iran, na kauli zake za kuingilia mambo ya ndani ya mataifa mengine zinaonyesha kwamba, lengo lake kuu limekuwa si kuwaunga mkono watu wa Iran bali kuendeleza maslahi ya kisiasa na kiuchumi ya Marekani na washirika wake. Kwa muktadha huo, madai kama hayo yanapaswa kutafsiriwa kama mazingaombwe ya kisiasa yanayoendana na malengo ya kiburi cha Marekani kuliko msimamo wa kibinadamu na nia ya dhati ya kiutu.