
Video ya WHO Kanda ya Afrika inaanzia nyumbani kwa Florida Nyirakarambe, mama wa makamo, ambaye maumivu yasiyokoma ya sehemu ya tumbo la chini yalibainishwa kuwa ni saratani ya shingo ya kizazi.
Anasema, “waliponiambia kuwa niña saratani, binafsi nilijua haiponyeki.”
Lakini uwekezaji wa Rwanda kwenye tiba dhidi ya saratani uliokoa maisha ya Florida kwani anasema, “walinishauri jinsi ya kumeza dawa zangu, na sikuziacha kabisa. Nilimeza kama walivyonishauri.”
WHO inasema Rwanda iko njiani kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi mwaka 2027, ambapo ni miaka mitatu kabla ya lengo la Umoja wa Mataifa. Je nini kimefanyika? Dkt. Augustin Katera ni Afisa wa WHO nchini Rwanda.
« Imekuwa ni jukumu la msingi kupatia kipaumbele utoaji wa chanjo dhidi ya virusi vya Human Papiloma, au HPV nchini ili kupunguza saratani ya shingo ya kizazi. »
Halikadhalika Kampeni za uchunguzi zinafanywa na wahumudu wa afya nchini kote waliopatiwa mafunzo.
Tangu mwaka 2018 Rwanda imechunguza asilimia 30 ya wanawake wanaopaswa kufanyiwa uchunguzi dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kati yao hao asilimia 90 wamepatiwa matibabu.
Rachel Uwimbabazi anaonekana akiingia hospitali kwa uchunguzi na anasema, « Nimesikia kuwa ikigundulika mapema inatibika na kupona. Ndio maana nimefika hapa kuchunguza mapema ili niepuke kuugua. »