Katika taarifa yao pamoja waliyoitoa hii leo huko Geneva Uswisi wataalamu huru  hao 14 wa Umoja wa Mataifa wameeleza kuwa kuna hali kubwa ya hofu nchini humo, inayochangiwa na tuhuma za watu kutoweshwa kwa nguvu, matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya wafuasi wa vyama vya upinzani, pamoja na kukandamizwa kwa vyombo vya habari na asasi za kiraia.

Tuhuma zilizotoewa

Kupitia tarifa hiyo wamesema mwenendo unaoonekana sasa unafanana sana na ule ulioshuhudiwa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2021, ambapo angalau watu 18 walithibitishwa kutoweka kwa nguvu.

Kwa mujibu wa taarifa yao, mwaka 2025 pekee, zaidi ya watu 160 waliripotiwa kutoweka, huku wakidaiwa kuchukuliwa na vyombo vya usalama kwa kutumia magari yasiyo na alama maalum na kushikiliwa katika vituo visivyojulikana.

Wataalamu hao pia wanaripoti kuwa vikosi vya usalama vimetumika kukandamiza mikutano ya chama kikuu cha upinzani cha National Unity Platform, kwa kutumia gesi za kutoa machozi, magari ya maji ya kuwatawanya waandamanaji, na hata risasi za moto, hali iliyosababisha kifo cha mtu mmoja kuthibitishwa.

Zaidi ya hapo, wanachama na wafuasi zaidi ya 550 wa upinzani wameripotiwa kukamatwa, huku Serikali ikilaumiwa kwa kushindwa kutekeleza kwa haraka uamuzi wa Mahakama ya Juu unaotaka kesi za kisiasa kuondolewa kwenye mahakama za kijeshi.

Kwa upande wa vyombo vya habari, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema uhuru wa habari na haki za kidijitali zimedhoofishwa, wakitaja kushambuliwa kwa waandishi wa habari, kusimamishwa kwa vipindi vya redio, kufutiwa vibali kwa waandishi, pamoja na matumizi ya sheria ya matumizi mabaya ya mitandao kuzima sauti za wakosoaji.

Pia kuna taarifa za upelelezi wa kidijitali, ikiwemo kudukuliwa kwa simu za wanaharakati na viongozi wa asasi za kiraia.

Wito kwa serikali

Wataalamu hao wamesema “Uchaguzi hauwezi kuchukuliwa kuwa huru na wa haki ikiwa haki za uhuru wa kukusanyika, kujumuika na kujieleza hazijahakikishwa kikamilifu. Kufunga nafasi ya upinzani kuna hatari ya kusababisha vurugu zaidi za uchaguzi.”

Wataalamu hao wameikumbusha serikali ya Uganda wajibu wake wa kuhakikisha wananchi wanashirika katika masuala ya umma bila ya kuwepo kwa vurugu wala kubaguliwa.

Wameeleza tayari wanawasiliana na serikali ya Uganda kuhusu masuala hayo na kwamba “Mamlaka lazima ifanye uchunguzi wa haraka, unaofaa, usioegemea upande wowote, huru na wa kina, ikiwawajibisha wahalifu na kuhakikisha kwamba waathiriwa wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu wanapata haki na fidia.”

Pia serikali iweke wazi hatima ya waliotoweka, kulinda uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kujiunga, na kuhakikisha uchaguzi unafanyika bila vitisho, vurugu wala kisasi.

Kuhusu wataalamu huru

Wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa, wanaojulikana kwa lugha ya kiingereza kama Special Rapporteurs, Independent Experts na Working Groups, ni wataalamu wa haki za binadamu wanaoteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Kwa pamoja, wanaitwa Special Procedures.

Wataalamu hawa wanafanya kazi kwa hiari bila mshahara, si wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, na hufanyakazi kwa uwezo wao binafsi.

Ingawa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa hutoa msaada wa kiutendaji, wataalamu hawa hawawakilishi serikali, taasisi wala Umoja wa Mataifa wenyewe, na maoni wanayotoa ni yao binafsi.

Wafuatilie mtandaoni kupitia @UN_SPExperts.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *