Chapisho katika wavuti wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF nchini Haiti, linaesema Dieussika, mwenye umri wa miaka 13, amekuwa akiishi kwa amani na familia yake kabla ya vurugu za kutumia silaha na ukosefu wa usalama kuwalazimisha kukimbia.
“Tulilazimika kuondoka nyumbani kwetu, na dada yangu kidogo afariki dunia kwa sababu ya pumu,” amesema.
Haiti bado iko katika mtego wa mgogoro mkubwa wa kiusalama, huku magenge yakipigania udhibiti wa maeneo katika mji mkuu na kwingineko.
Ukosefu wa usalama umesababisha mamia ya maelfu ya watu kuyahama makazi yao, hali iliyoongeza matatizo ya kibinadamu na kiuchumi ambayo nchi inakabiliana nayo.
Migogoro, uhamaji wa lazima, umaskini na ukosefu wa usalama vimeungana na kufanya elimu kuwa karibu haiwezekani kwa mamia ya maelfu ya watoto wa Haiti.
Kufungwa kwa shule
Katika mwaka wa masomo wa 2024–2025, shule nyingi ziliathiriwa vibaya moja kwa moja na vurugu, huku zaidi ya shule 1,600 zikifungwa na kadhaa zikichukuliwa na makundi yenye silaha.
Katika makazi ya muda na vituo vya wakimbizi vilivyojaa kupita kiasi, watoto hawana vitabu, vifaa vya kujifunzia wala walimu wenye sifa.
Familia wapata hifadhi ndani ya jengo la shule huko Port-au-Prince, Haiti.
Makazi ya muda
Familia ya Dieussika imelazimika kuishi katika maeneo kadhaa ya muda, lakini maisha yameendelea kuwa magumu. Anasema kuna magonjwa, wadudu wanaong’ata, lakini licha ya yote, anataka kuendelea na masomo.
Akiwa katika moja ya vituo vya watu waliokimbia makazi yao, Dieussika ameweza kurejea masomoni kupitia madarasa ya kurejesha masomo yaliyoandaliwa na UNICEF.
Leo, ana ndoto ya kuwa mtu muhimu katika jamii ili kuwasaidia watoto na kuwaelimisha vijana kuhusu kukataa vurugu za kutumia silaha.
Shule ni nguzo ya matumaini wa maisha
Usiku mmoja, mvua kubwa ililowesha mali zake, ikaharibu vitabu na sare zake za shule. Hata hivyo, Dieussika alikesha usiku kucha akivikausha, akiwa na azma ya kutokata tamaa na masomo yake.
“Elimu ina maana kubwa sana kwangu. Bila elimu, ndoto yangu ingepotea,” amesema.
Masomo anayoyapenda zaidi ni Kifaransa na hisabati, na anasema huhisi fahari kila anapopeleka nyumbani matokeo mazuri kwa wazazi wake.
Kupitia miezi mitano ya madarasa ya kurejesha masomo kwa msaada wa taasisi ya kiraia ya Education Cannot Wait, inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Dieussika ameweza kufanya mitihani yake na kurejea shuleni.
“Nilikuwa nimepoteza matumaini, lakini madarasa haya yalinirejeshea imani. Pia tulipata mafunzo ya ufundi kama ushonaji wa crochet, utengenezaji wa bidhaa za ngozi na urembo. Ilikuwa fursa ya kipekee,” amekumbuka kwa fahari.
Dieussika anaonesha familia yake kazi zake za shule za kufanywa nyumbani.
Bila elimu ndoto hazitatimizwa
Shuleni, Dieussika hushiriki kikamilifu katika darasa la hisabati, akitiwa moyo na kuungwa mkono na mwalimu wake. Anataka kukomesha ugumu unaoikabili familia yake na kuwaonesha kuwa nao wanaweza kufuata nyayo zake.
“Nataka kuwa mtu muhimu ili kuwasaidia watu. Bila shule, hatuwezi kutimiza ndoto zetu,” amesema kwa msisitizo.
Ujumbe wake kwa watu wazima na watoa maamuzi ni wazi na wenye kugusa mioyo:
“Msikate tamaa kwa watoto. Wapendeni zaidi na wape fursa za kujifunza na kuota ndoto.”
Wasichana wengi balehe kama Dieussika huacha shule kutokana na hofu ya usalama, majukumu ya kuwahudumia wengine au ukosefu wa vifaa vya usafi wa hedhi.
Kukimbia vurugu hakukuizuia mapenzi ya Dieussika kwa elimu
Kupitia kazi ya Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na mamlaka za Haiti na washirika, programu za msaada wa kielimu na kisaikolojia zimewafikia zaidi ya watoto 17,500, wakiwemo wasichana 10,500.
Kwa Dieussika, kama ilivyo kwa wengi wengine, programu hizi ni zaidi ya elimu ni njia ya kuokoa maisha, fursa ya kubadili hofu kuwa imani na malengo makubwa.