Dar es Salaam. Kwa bahati mbaya kuna vitabu vichache sana vinavyozungumzia historia ya muziki wa dansi na Taarab Tanzania.

Bahati mbaya hata hivyo vichache karibu vyote vimeandikwa na watu kutoka nje ya Tanzania. Kutokana na kukosekana kwa kumbukumbu hizo, taratibu unaona jamii ikisahau mchango mkubwa ambao wanamuziki walichangia katika kulifanya Taifa hili kuwa lilipo.

 Muziki wa dansi, Taarab na kwaya ulihamasisha sana kukua kwa lugha ya Kiswahili, muziki huu ulisaidia kuondoa tofauti za ukabila, muziki huu ulitumika kusambaza ujumbe wa kudai Uhuru na hata mara nyingine maonyesho ya muziki huu yalitumika kama nafasi ya kuficha mikutano waliokuwa wakifanya viongozi katika kutafuta Uhuru wa nchi hii. 

Matamko ya viongozi wengi wa sasa, hata wale wenye uzalendo mkubwa bado yanaonyesha kutokuwa na taarifa ya historia ya mchango wa muziki wa dansi na taarab katika historia ya nchi hii.

Wanamuziki walianza kutunga nyimbo ambazo zilielezea hali halisi na hata kutabiri nchi yetu kupata Uhuru miaka kadhaa kabla ya nchi kupata Uhuru, nyimbo nyingine ziligeuka kuwa shubiri kwa utawala wa wakoloni kiasi cha kusakwa kwa udi na uvumba na kuharibiwa.

 Santuri za wimbo  wa Marehemu Frank Humplick na Dada zake  ulioitwa ‘I am a democrat’ au wengi waliufahamu kwa jina la ‘English yes no, kizungu sikijui’, ilikuwa moja ya santuri ambazo zilisakwa nyumba kwa nyumba na kuvunjwa, kwa kuwa zilionyesha kuhamasisha wananchi kutafuta Uhuru toka kwa wakoloni.  

Katika uchaguzi wa kwanza wa nchi hii, taratibu zilihamasisha kila jimbo kuwa na wagombea watatu kwa kila jimbo, Mwafrika, Muhindi na Mzungu. Salum Abdallah na kundi lake la Cuban Marimba Band walitunga wimbo ambao ulikuwa na maneno haya;
Siku moja nilipita barabarani,

Nikawa wakuta kuku watatu wanapigana,
Kuku mweusi anampiga kuku mweupe,
Kuku mweupe anampiga kuku mwekundu
Kuku mwekundu anapiga kuku mweusi
Wimbo huu nao ulileta tafrani kwa mkoloni, kwa kuonyesha picha hii ya uchaguzi ilivyokuwa. 

Lakini Mungu mkubwa hatimaye tulipata Uhuru na bendi nyingi sana zilitunga nyimbo kuhusu furaha ya kupata Uhuru. Kwa miaka mingi baada ya hapo, vijana wengi waliokuwa wazalendo na walitunga nyimbo ambazo mpaka zama hizi bado nyimbo hizo zina hamasisha uzalendo, na kuonyesha historia ya hali ilivyokuweko wakati huo.

 Karibu kila mpenda muziki anaufahamu wimbo wa Tanzania yetu ndio nchi ya furaha uliorekodiwa mwaka 1967. Lakini bado unarekodiwa na vijana wa kizazi hiki.

Baada ya Uhuru wanamuziki walitegemea sana Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC) ambayo baada ikaja kuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kwa ajili ya kurekodi nyimbo zao. 

Kulikuweko na masharti ya kurekodi katika studio za redio hii ya Taifa, kati ya masharti yaliyokuweko ni yale yaliyoelekeza kuwa nyimbo zote kabla hazijarekodiwa RTD, mashahiri yake ilikuwa lazima yapelekwe kuhakikiwa na kamati ya RTD, na hapo maneno yalichujwa na hatimae nyimbo ambazo ziliruhusiwa kurekodiwa zilipitishwa na zile zenye utata aidha zilikataliwa au wanamuziki walishauriwa kuzifanyia mabadiliko, na ilitokea hata mara nyingine nyimbo ambazo zilipitia mchujo huu zilikuja baadae kuzuiliwa kurushwa hewani. 

Sharti jingine lilihusu bendi za Kikongo, ambazo  zilipewa masharti ya kuanza kurekodi nyimbo kwa lugha ya Kiswahili, kwani wakati huu bendi nyingi za Kikongo zilitunga nyimbo zao kwa lugha yao ya Kilingala, mara nyingine yenye maneno machache ya Kifaransa. 

Sharti  jingine lilikuja kutolewa, ni kuwa kila bendi inapokwenda kurekodi ni lazima kuweko na wimbo mmoja au zaidi wa kizalendo au wenye ujumbe kwa jamii, sharti hilo ndilo lililofanya kuweko na nyimbo nyingi sana za kizalendo zilizotungwa na wanamuziki wa Kitanzania.

Pia kulikuweko na maazimio, matamko ya serikali, kampeni mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa,  hata matukio makubwa na kwa yote hayo vikundi vya muziki vilihamasishwa kutunga na kurekodi nyimbo, nyimbo ambazo kwa sasa zimekuwa ni kigezo cha kuonyesha kuwa vijana zamani walikuwa watunzi wa nyimbo za kizalendo. 

Masharti yaliyowekwa kabla ya kurekodi nyimbo baadae yaligeuka kuwa jambo la kawaida kwa wanamuziki na wananchi na hivyo nyimbo za kizalendo zilitungwa bila shinikizo kutoka nje ya wasanii wenyewe. Na wapenzi wa muziki walizipokea nyimbo hizo kwa kutegemeana na ubora wa wa muziki ulivyopangwa na kupigwa.

Labda nizungumzie nyimbo chache za aina hii ambazo binafsi nilishiriki. Mwaka 1988 nikiwa katika bendi ya TANCUT Almasi, marehemu Mzee Zacharia Daniel aliyekuwa maarufu kwa jina la Zacharia Tendawema,  alitunga wimbo ulioitwa Kuwajibika, waimbaji katika wimbo huo walikuwa Mzee Daniel Tendawema, mapacha Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa, Hashim Kasanga na Mohamed Shaweji.

Marehemu Zacharia alipewa jina la Tendawema kutokana na kutunga wimbo Tenda wema uende zako aliyoutunga na kuuimba akiwa na Shinyanga Jazz Band.

Nilihama kutoka bendi ya TANCUT mwaka 1989  na kwenda Vijana Jazz Band, huko nilishiriki nyimbo nyingi sana kutunga, kuimba na kupiga gitaa katika nyimbo zenye ujumbe mbalimbali.

Lakini niongelee wimbo wa Nelson Mandela. Bendi nyingi za Tanzania zilihamasika kutunga nyimbo za Mandela kutokana na ziara ambayo Rais Nelson Mandela alikuja kuifanya Tanzania kama shukrani yake kwa Watanzania kwa kuunga mkono mapambano dhidi ya ukaburu.

Wimbo huo tulioufanyia mazoezi usiku kucha  na kwenda kuurekodi RTD, ulikuwa ndio wimbo wa mwisho ambao  Hemed Maneti aliurekodi kabla ya kifo chake.   

Bendi iliupiga wimbo huo mbele ya Nelson Mandela mwenyewe alipohutubia uwanja wa Jamhuri Dodoma, uwanja wa  Jamhuri Morogoro, na mwisho tulipiga mbele yake Uwanja wa Taifa tukiwa na bendi ya Washirika Tanzania Stars ambayo nayo ilikuwa na wimbo wa Mandela uliokuwa ukiimbwa na Eddy Sheggy.

Nyimbo hizi za kizalendo sio tu zilihamasishwa kutungwa lakini pia RTD ilihakikisha kuwa inazirusha nyimbo hizo hewani, hivyo zilikuja kujulikana na kupendwa. 

Pamoja na kuwa kuna radio nyingi sana siku hizi, nafasi ya kusikika hewani nyimbo za kizalendo siku hizi ni finyu sana, kisingizio huwa mara nyingi kuwa redio hizo zinaendeshwa kibiashara. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *