Serikali ya Zanzibar, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imeanza kufanya maboresho ya miundombinu ya usafiri wa baharini na kuchochea ukuaji wa uchumi wa visiwa hivyo kupitia ujenzi wa kituo kipya cha abiria cha kivuko cha Maruhubi(Mpiga Duri)
Mradi huo unatekelezwa kwa miaka mitatu kwa mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kati ya Shirika la Bandari Zanzibar na Kampuni ya Zanzibar Ferry Development Company Limited, na unatarajiwa kugharimu zaidi ya dola milioni 400, ambapo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ni mmoja wa wafadhili wakuu wa mradi huo.
Kituo hicho kitakachohudumia abiria takribani 8,000 kwa siku kitajumuisha vivuko vya abiria, vivuko vya kasi, meli za Roll-on/Roll-off pamoja na teksi za baharini. Pia kitajumuisha eneo la bidhaa zisizotozwa ushuru (duty-free), maduka ya rejareja na kituo cha ndege za baharini (seaplane), hatua itakayoiimarisha Zanzibar kama kitovu cha kikanda cha usafiri wa baharini na utalii.
Mkurugenzi Mkuu wa Zanzibar Ferry Development Company, Jaffer Machano, ameishukuru NBC kwa mchango wake mkubwa, akisema ushirikiano huo ni nyenzo muhimu katika kusukuma mbele uchumi wa visiwa hivyo.
NBC inaendelea kushiriki katika miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo kuwa mwezeshaji mkuu wa mkopo wa dola milioni 200 kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufadhili miradi ya kijamii na kiuchumi.
#AzamTVUpdates
Mhariri | John Mbalamwezi