Rose Muhando alia na Sony Music Africa, Seven atia nenoRose Muhando alia na Sony Music Africa, Seven atia neno

Dar es Salaam. Mwanamuziki wa nyimbo za injili nchini Rose Muhando amedai kampuni inayojihusisha na uuzaji na kusambazaji wa muziki ‘Sony Music Africa’ imekuwa ikimdhulumu haki yake kwa takribani miaka 15 sasa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Rose amedai licha ya kusitisha mkataba wa kufanya kazi na kampuni hiyo, lakini bado imekuwa ikishikilia nyimbo zake zaidi ya 37.

“Ni muda mrefu sana umepita takribani miaka 15 nimekuwa nikinyamaza. Nikivumilia kwa moyo wote, nikiamini haki yangu nitaipata lakini leo, maumivu yamenilazimu kufungua mdomo na kusema.

“Kwa muda mrefu sasa, nimekuwa nikidhulumiwa haki yangu ya mapato kutokana na kazi zangu katika majukwaa yote ya kidijitali. Haya yote yametokana na ushirikiano wangu wa zamani na kampuni ya Sony Music Africa licha ya kwamba tulishaacha kufanya kazi pamoja kitambo.

“Hadi leo kampuni hiyo bado inashikilia zaidi ya kazi zangu 37, na inakataa kuziaachia. Cha kusikitisha zaidi, sipati hata shilingi moja kutokana na kazi hizo ambazo ni jasho langu, jasho la maisha yangu,”ameandika

Aidha msanii huyo ameongezea kwa kueleza Serikali kupitia Cosota Tanzania imejaribu kumsaidia na kusimamia haki zake, lakini juhudi hizo zimekwamishwa kwa kukosa ushirikiano kutoka kwa mwakilishi wao Seven Mosha.

“Amekuwa akiitwa mara kadhaa bila kutoa ushirikiano wowote. Hali hii imeniumiza sana, imenivunja moyo, na inarudisha nyuma ndoto za wasanii wengi ambao kimyakimya wanaendelea kudhulumiwa haki zao.

Seven Mosha Mwakilishi wa Sony Music Afrika Mashariki

“Kwa unyenyekevu mkubwa, naomba Serikali kupitia Waziri wetu, mheshimiwa Paul Christian Makonda uingilie kati suala hili kwa haraka. Naomba haki itendeke. Naomba jasho la msanii liheshimiwe, naomba ndoto zetu zisizidi kukandamizwa Basata, Cosota Tanzania nimechoka kuvumilia nimechoka kunyamaza naomba haki,”ameandika Rose Muhando

Hata hivyo, Mwananchi ilipojaribu kumtafuta  kwa njia ya simu Seven Mosha ambaye ni Mwakilishi wa Sony Music Afrika Mashariki, alijibu kwa kifupi kuwa “hakuna kitu kama hicho” kisha akakata simu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *