Marekani. Nyumba, magari, mavazi, mahusiano na vinginevyo ni miongoni mwa vitu ambavyo wasanii na watu maarufu duniani hupenda kuonyesha mitandaoni kama sehemu ya kujenga taswira ya maisha yao.

Mitandao ya kijamii imegeuka kuwa majukwaa ya kuonyesha utajiri, mafanikio na anasa, huku kila chapisho likiwa na ujumbe kwa mashabiki kuhusu maisha wanayoishi mastaa.

Hata hivyo, siyo kila msanii hufanya hivyo, wapo wanaoamini umaarufu haupimwi kwa vitu unavyoonyesha, bali kwa kazi unayoifanya na mizizi unayoitambua.  Miongoni mwa majina yanayokwenda kinyume na mtazamo huo ni rapa maarufu wa Marekani, Marshall Bruce Mathers maarufu Eminem (53), aliyeanza fani hiyo miaka ya 1988.

Licha ya kuwa miongoni mwa wasanii wanaouza zaidi katika historia ya muziki wa dunia na kujikusanyia utajiri unaokadiriwa kufikia dola milioni 250, Eminem ameendelea kuishi maisha ya kawaida.

Tofauti na mastaa wengi wa hip hop wanaopenda kuonyesha majumba makubwa na maisha ya kifahari mitandaoni, The Real Slim Shady amebaki jijini Detroit, mji uliopo Michigan, Marekani, mahali alipoanzia safari ya muziki.

Eminem ana utajiri unaokadiriwa kufikia Dola 250 milioni (zaidi ya Sh550 bilioni) na anatambuliwa kama mmoja wa wasanii wanaouza zaidi katika historia ya muziki akiwa ameuza zaidi ya rekodi milioni 220 duniani, na nakala milioni 228.5 zilizothibitishwa nchini Marekani. Rapa huyo mshindi wa Tuzo ya Oscar amenunua nyumba tatu hadi sasa akichagua mtindo wa maisha wa kawaida kuliko anasa za kupindukia kama ilivyo kwa mastaa wengine.

Eminem bado anaishi Detroit na hajununua nyumba nyingine kwa zaidi ya miaka 20 sasa ikiwa ni ishara ya uhusiano wake wa dhati na mji anaouita nyumbani. Kwa sauti kali na mashambulizi ya maneno, Eminem alivunja mipaka ya muziki wa hip-hop uliokuwa ukitawaliwa na wasanii weusi akageuza maumivu kuwa mashairi yenye nguvu.

Kuanzia Infinite yenye makali ya uhalisia hadi ukali wa The Slim Shady LP, safari yake imekuwa ya kasi na nidhamu.

Baada ya kusainiwa na Dr Dre kupitia Aftermath Entertainment mwishoni mwa miaka ya 1990, Eminem aligeuka kuwa mmoja wa wasanii waliopata mafanikio makubwa zaidi katika historia ya hip-hop.  Ameachia albamu 12 na EP moja.

Kwa takwimu, anatajwa miongoni mwa wasanii wanaouza zaidi duniani, huku The Eminem Show ikiwa albamu ya hip-hop iliyouza zaidi katika historia. Licha ya utajiri na umaarufu, Eminem amebaki kuwa mtu wa kawaida. Tofauti na mastaa wengi, hajakimbilia kununua majumba mengi kwa zaidi ya miongo miwili akibaki na makazi yaleyale.

Makala haya ya maisha ya Eminem nje ya muziki inaeleza nyumba alizomiliki, falsafa ya maisha na sababu zilizomfanya achague kuishi tofauti licha ya mafanikio makubwa.

EMI 05

1. Jumba la Oakland Township, Detroit

Mwaka 2003, Eminem alinunua jumba la kifahari Oakland Township kwa Dola 4.75 milioni. Nyumba hiyo ya mita za mraba 1,625 ilikuwa kwenye ekari sita zenye ulinzi mkali ikiwa na njia za matembezi, uwanja wa michezo, bwawa, maporomoko ya maji na spa.

Kulikuwa pia na nyumba ya wageni yenye chumba cha michezo, vyumba vitano vya kulala vyenye mabafu ya ndani, mabafu 10 na lifti aliyotaja hata kwenye wimbo wake. Humo ndimo alikulia binti zake watatu, akiwemo Hailie Scott ambaye sasa ameolewa na kumfanya Eminem kuwa babu.

Baada ya zaidi ya miaka 10, aliuza jumba hilo mwaka 2017 kwa Dola 1.9 milioni chini ya nusu ya bei aliyolinunua.

EMI 01

2. Makazi Makuu, Detroit

Septemba 2000, mshindi huyo wa Tuzo 15 za Grammy alinunua nyumba katika Clinton Township yenye thamani ya zaidi ya Dola 1.5 milioni. Nyumba hiyo ya mita za mraba 836 iko kwenye jumuiya iliyofungwa kaskazini-mashariki mwa Detroit, ikiwa na vyumba vinne vya kulala na mabafu sita.

Ilijumuisha dari ndefu, mapambo ya taji, milango ya kioo, mahali pa moto matatu, baa ya ndani, mifumo ya sauti na usalama, chumba cha jua, eneo la kifungua kinywa na ofisi.

EMI 02

3. Makazi ya Sterling Heights, Detroit

Mwaka 1999, Eminem na aliyekuwa mke wake Kim Scott walinunua nyumba ya miaka ya 1980 huko Sterling Heights kwa dola 450,000. Nyumba hiyo ilikuwa na takribani futi mraba 5,000 kwenye ekari 2.78. Walifanya ukarabati wa jikoni na chumba kikuu cha kulala, huku zulia la rangi ya zambarau likivutia macho.

Umaarufu uligeuka usumbufu mashabiki na wavamizi walifika mara kwa mara na baadhi ya vitu kwenye nyumba hiyo viliripotiwa kuibiwa. Eminem aliondoka mwaka 2001, akaiweka mnadani nyumba kwa Dola 750,000 lakini ikauzwa kwa Dola 475,000.

EMI 03

4. Nyumba ya Utotoni, Detroit

Nyumba ndogo ya matofali yenye vyumba viwili katika mtaa wa Dresden Avenue ina ukubwa wa futi mraba 767, lakini uzito wake wa kihistoria ni mkubwa.

Eminem alikaa kwenye ngazi zake za zege kwa jalada la The Marshall Mathers LP mwaka 2000, na kuifanya nyumba hiyo kuwa alama kwa mashabiki duniani.

Iliwakilisha zaidi ya makazi ilikuwa ishara ya maisha magumu yaliyomlea na kumpa sauti. Miaka michache baadaye, Eminem alisema alikuwa akirejea hapo mara kwa mara kukumbuka alikotoka.

Nyumba hiyo ilionekana tena kwenye jarida la The Marshall Mathers LP 2 (2013), safari hiyo ikiwa imeharibika. Baada ya kuungua kwa moto na kuonekana hatarishi ilibomolewa mwaka huohuo na 2022 Shirika la Detroit lilitangaza kubadili eneo hilo kuwa hifadhi ya nyuki.

EMI 04

KUMBUKUMBU ZA UMASKINI

Chanzo kikubwa cha mtazamo wa Eminem kuhusu maisha kinatokana na alikotoka. Alikulia katika mazingira magumu ya Detroit, akihama hama na mama yake, akiishi kwenye nyumba ndogo zilizozungukwa na umasikini, vurugu na kukata tamaa.

Maisha hayo yalimjenga kisaikolojia na kumfundisha kuthamini vitu vidogo. Kwa Eminem, Detroit si tu mahali pa kuzaliwa, bali ni alama ya mapambano yake. Ndiyo maana licha ya uwezo wa kuishi Los Angeles, New York au Miami, amechagua kubaki Detroit kama njia ya kujikumbusha safari yake.

EMI 06

Tofauti na wasanii wengi wanaoutumia umaarufu kama njia ya kuhalalisha anasa, Eminem anaonekana kuuona umaarufu kama chombo cha kazi, si lengo la maisha.

Kwa mtazamo wake, muziki ndio msingi wa kila kitu siyo kamera wala mitandao ya kijamii. Hii ndiyo sababu hana uwepo mkubwa mitandaoni na hapendi kuonyesha maisha binafsi ikiwa ni mara chache sana hutoa taswira ya familia au mali zake. Eminem anaamini msanii anapaswa kuzungumza kupitia kazi na siyo vitu anavyomiliki.

EMI 07

SABABU MAISHA YA FARAGHA

Kuna sababu kadhaa zinazomfanya Eminem aishi maisha ya kujitenga. Kwanza ni usalama wa familia akiwa baba na sasa babu, ameweka kipaumbele kwenye ulinzi wa watoto wake dhidi ya madhara ya umaarufu.

Pili ni afya ya akili amewahi kufanya mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari Marekani na kueleza hali hiyo ilimfanya atafakari upya maana ya maisha.

Maisha ya kelele na anasa kwake ni vishawishi vinavyoweza kumrudisha nyuma. Tatu ni nidhamu ya kazi anaamini utulivu humsaidia kuandika, kufikiria na kuendelea kuwa msanii bora.

EMI 08

Mkali huyo amefanya kazi mbalimbali, lakini baadhi zilizofanya vizuri ni pamoja na The Eminem Show (2002), albamu ya nne ya studio ya Eminem, ambayo bado inakikumbukwa kama albamu ya hip hop iliyouza zaidi.

Ilipata mauzo makubwa duniani, na kubadilisha mtazamo wa muziki wa hip hop baadhi ya nyimbo zilizovuma ndani ya albamu hiyo ipo Without Me, Cleanin’ Out My Closet, Sing for the Moment. Mbali na mapato aliyoingiza lakini albamu hiyo ilimpa tuzo nyingi za Grammy ikiwemo Best Rap Album.

Nyingine ni The Marshall Mathers LP (2000), albamu iliyomfanya Eminem kuwa nyota wa kimataifa aliuza zaidi ya nakala milioni 22 na baadhi ya nyimbo zilizofanya albamu hiyo kuwa maarufu ni pamoja na The Real Slim Shady, Stan, The Way I Am. Ikachukua tuzo ya Grammy kama Best Rap Album, na tuzo mbalimbali za MTV na Billboard albamu hiyo ilikuwa na nguvu kubwa ya kuvutia hadhira kubwa duniani, na kuingiza watazamaji bilioni moja.

Nyimbo nyingine zilizompa umaarufu mkubwa Eminem ni Not Afraid, Love the Way You Lie aliyomshirikisha Rihanna ambazo zote mbili zilitoka kwenye albamu yake ya Recovery (2010) iliyoshinda tuzo mbalimbali za Grammy, American Music Awards, Billboard Music Awards na nyinginezo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *