Dar es Salaam. Ni vipi Nandy atatekeleza ahadi yake 2026? Ndilo swali la mashabiki wengi mara baada ya staa wa Bongo Fleva, Nandy kutangaza anatarajia kutoa albamu mbili mwaka huu wa 2026, huku akiwa hana rekodi ya kuwahi kufanya hivyo.
Kauli ya Nandy, mkali wa kibao maarufu kinachokwenda kwa jina la Dah! (2024), inakuja baada ya kushindwa kuachia albamu yake ya pili mwaka uliopita kama alivyokuwa ameahidi hapo awali.
Albamu yake ya kwanza, The African Princess (2018) ilitoa nyimbo maarufu kama Aibu na Hazipo, huku ukijumuisha ambazo tayari zilikuwa zimetoka awali – One Day, Wasikudanganye, Kivuruge na Ninogeshe.
“Naona comments nyingi DM zikiniuliza kuhusu albamu. Tunatoa albamu mbili mwaka huu; ya kwanza baada ya Ramadhan, na ya pili mwishoni mwa mwaka 2026 tukijaliwa uhai,” alisema Nandy kupitia Insta Story na kuongeza.
“Lakini mwezi huu kuna wimbo mpya (new hit song) unakuja hivi karibuni,” alieleza Nandy, mshindi wa tuzo za All Africa Music Awards (AFRIMA) 2017 & 2020.
The African Princess huyo anakuja na albamu mpya tena mbili ikiwa ni takribani miaka minane imepita tangu alipoachia albamu yake ya mwisho ambayo ilitoka chini ya usimamizi wa Epic Records.
Pengine anafanya hivyo baada ya kuona amewasubirisha mashabiki wake kwa muda mrefu, hivyo sasa anataka kuikata kiu yao kwa burudani ya kiwango cha juu zaidi ambacho hakijazoeleka kutoka kwake.
Taarifa ya kuachia albamu mbili ndiyo imeongeza mshawasha kwa mashabiki wake wengi na sasa utekelezaji ndio unasubiriwa. Je, atafanya kama alivyoahidi?, au yatakuwa yale yale ya mwaka uliopita?. Yetu macho na masikio.
Hata hivyo, ikumbukwe kuwa Nandy alishawahi kufanya jambo sawa na hilo takribani miaka minne nyuma na alipata matokeo mazuri katika kazi yake.
Ni pale alipoachia E
xtended Playlist (EP) zake mbili, Taste (2021) na Wanibariki (2021) yenye muziki wa Injili pekee, na hadi sasa imesikilizwa (streams) mara milioni 5.4 katika mtandao wa Boomplay.
EP yake ya Injili (Wanibariki), ilikuja kukumbushia kile alichofanya katika cover ya wimbo wa Angel Benard, Nikumbushe (2018), mradi ulioshinda Maranatha Awards 2018, tuzo zinazotolewa Kenya.
Lakini kwa mwaka huu anakuja na albamu mbili, zote zikibeba maudhui ya aina moja – muziki wake wa kila siku wa kidunia (secular music) na hapo ndipo inaonekana kazi kubwa iliyo mbele yake.
Hata hivyo, ni muda mrefu tangu ametoa albamu (The African Princess – 2018), na hata EP (Maturity – 2022), hivyo kuna uwezekano mkubwa amefanya matayarisho kwa muda mrefu.
Nandy si mwanamuziki pekee wa Bongofleva aliyedokeza kuachia albamu mwaka huu, kuna Zuchu ambaye hiyo itakuwa ni albamu yake ya pili baada ya hapo awali kutoa – Peace and Money (2024).
Wasanii hawa wamekuwa wakiwekwa katika mzani sawa wa kiushindani na kundi kubwa la mashabiki lililopo nyuma yao, hivyo iwapo wataachia albamu kwa wakati mmoja tutegemee pande zote kupeana changamoto.
Hiyo itakuwa ni albamu ya kwanza kwa Nandy tangu kushinda tuzo nne za Muziki Tanzania (TMA) 2021 & 2023 akiwa ni msanii wa pili wa kike aliyeshinda mara nyingi zaidi tangu msimu wa 2021.
Nandy ameshinda vipengele vingi vikubwa katika TMA kama Msanii Bora wa Kike lakini cha Albamu Bora ya Mwaka ndio bado na hajawahi kuwania, hivyo huwenda miradi hiyo ikampa nafasi hiyo.
Mumewe Billnass ambaye hakushiriki katika albamu ya kwanza wala katika EP zote tatu, ni kati ya wasanii wenye asilimia kubwa ya kusikika katika albamu hizo za Nandy.
Mastaa hao waliofunga ndoa Juni 2022, tayari wameshirikiana katika nyimbo tano – Bugana (2019), Do Me (2020), Party (2021), Bye (2022) na Totorimi (2024), huku zote kwa sehemu kubwa zikifanya vizuri.
Hata hivyo, Nandy anaelekea kukamilisha albamu tatu huku pia akiwa na EP tatu, lakini Billnass aliyetoka na wimbo wake, Raha (2014) chini ya Rada Entertainment, hajawahi kutoa EP wala albamu!
Pengine albamu hizo za Nandy zitaweza kumuamsha Billnass na kumkumbusha kuhusu hilo. Ni mara chache sana msanii kuwepo katika muziki kwa miaka zaidi ya 10 akifanya vizuri bila kutoa albamu.
Ikumbukwe baadhi ya wasanii wa Bongo Fleva waliotoa albamu mwaka uliopita, ni Darassa (Take Away The Pain), Jay Melody (Addiction), Lady Jaydee (Silver), Moni Centrozone (Watoto wa Mtaani) n.k.
Kwa upande wa EP kulikuwa na Nedy Music (The Voice of The Island), Lava Lava (Time), Yammi (After All), Phina (Melanin Therapy), Jux (A Day To Remember), Mbosso (Room Number 3) n.k.