
Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi Kamishina Mkuu huyo amesema “Haya yanatokea wakati wananchi wa Ukraine wanakabiliwa na baridi kali, huku viwango vya joto vikishuka hadi chini ya nyuzi joto -10 za Selsiasi wakati wa usiku”.
Türk ameendelea kusema kuwa, “ raia ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa mashambulizi haya. Hayana maelezo mengine isipokuwa ukatili. Lazima haya yakomeshwe. Kulenga raia na miundombinu ya kiraia ni ukiukaji wa wazi wa sheria za vita.”
Mashambulizi ya jana usiku yaliyotumia silaha za masafa marefu na yamesesababisha kukatika kwa dharura kwa umeme na joto katika maeneo kadhaa. Katika Jiji la Kyiv, meya ameripoti kuwa majengo ya makazi ya ghorofa 5,635 yalibaki bila vipasha joto asubuhi ya leo, karibu asilimia 80 kati yake yalikuwa yameanza tu kurejeshewa huduma ya vipasha joto baada ya kukatika kufuatia shambulizi kama hilo tarehe 9 Januari.
Maelfu ya familia hawana vipasha joto
Türk anasisitiza kwamba hii ina maana kuwa mamia ya maelfu ya familia sasa hawana joto, na maeneo kadhaa, ikiwemo sehemu kubwa ya Kyiv, pia hayana maji. Hali hii inaathiri zaidi makundi yaliyo hatarini, wakiwemo watoto, wazee na watu wenye ulemavu.
Türk amesema kuwa Shirikisho la Urusi limeendelea kutekeleza mashambulizi haya makubwa licha ya kuwepo kwa taarifa nyingi za wazi na zilizothibitishwa zinazobainisha madhara makubwa kwa raia.
Tangu Oktoba mwaka jana, majeshi ya Urusi yameanzisha upya mashambulizi makubwa na ya kimfumo dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine, huku mashambulizi yakiripotiwa katika angalau mikoa 20 nchini humo.
Kufuatia mashambulizi kama hayo mwaka wa 2024, mashambulizi haya yamedhoofisha kwa ujumla mfumo wa nishati wa Ukraine, hali iliyosababisha kukatika kwa umeme kwa zamu katika maeneo mengi ya nchi, mara nyingi kwa hadi saa 18 kwa siku katika miezi ya hivi karibuni.
Türk ametoa wito kwa mamlaka za Urusi kusitisha mara moja mashambulizi haya. Kwa kuwa inasikitisha sana kuona raia wakiteseka kwa namna hii.