
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov amesisitizia tena haki ya Iran ya kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani.
Lavrov ametoa sisitizo hilo alipohutubia mkutano na waandishi wa habari uliopewa jina la “Matokeo ya Diplomasia ya Russia Mwaka 2025,” ambapo sambamba na kuashiria tena misimamo ya nchi yake kuhusu suala la nyuklia la Iran amesisitiza kuwa, haki ya Tehran ya kutumia nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya amani lazima iheshimiwe.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametoa mjibizo pia kwa majaribio ya baadhi ya nchi za kigeni ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran na akasema: “majaribio ya nje ya kudhoofisha sera za kigeni za Iran yanatia wasiwasi sana.”
Akijibu suali kuhusu matarajio ya baadaye katika uhusiano wa kibiashara kati ya Russia na Iran baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuweka ushuru wa asilimia 25 kwa nchi yoyote inayofanya biashara na Iran, Lavrov amesema: “uhusiano na biashara kati ya Russia na Iran zitaendelea.”
Amefafanua kwa kusema: “tuna mipango mizuri ya ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, si tu katika biashara, bali pia katika uga wa uwekezaji.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameelezea kusikitishwa na namna sheria zote zilivyowekwa kando katika jukwaa la kimataifa.
Amesisitiza kwamba mchezo wa “nguvu ndizo zinazoamua haki” ndio unaochezwa hivi sasa katika uwanja wa kimataifa.
Lavrov amebainisha hilo kwa kusema: “tunashuhudia mabadiliko makubwa katika nidhamu nzima ya dunia; hii inaonyesha kwamba, Magharibi, ambayo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, ilikuja na dhana yake ya nidhamu ya dunia inayosimama juu ya msingi wa sheria, sasa imeamua kukabiliana kikamilifu na sheria za kimataifa katika tafsiri na misingi yake”.
Ameongezea kwa kusema: “hii inaonyesha wazi kuwa msamiati huu sasa umeshafutwa kikamilifu”…/