
Rais wa Marekani Donald Trump amemkosoa vikali Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa kukataa kujiunga na kile kinachoitwa “Bodi ya Amani” ya Washington kwa ajili ya Ghaza, huku mpango huo ukikabiliwa na ukosoaji mkubwa wa wataalamu wa sheria za kimataifa wanaouelezea kuwa ni upanuzi wa ukaliaji wa mabavu wa eneo hilo la Palestina unaofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel.
Alipoulizwa siku ya Jumanne na waandishi wa habari kuhusu msimamo wa Macron wa kukataa kujiunga na ‘Bodi ya Amani ya Ghaza’ Trump alitoa maanani umuhimu wa kiongozi mkuu huyo wa Ufaransa huku akitilia shaka mustakabali wake wa kisiasa.
“Hakuna anayemtaka kwa sababu ataondoka madarakani hivi karibuni,” Trump alisema.
Aidha, alionya kwamba ikiwa Ufaransa itachukua msimamo wa kiuadui kuhusiana na mpango huo, ataweka “ushuru wa 200% kwa bidhaa za mvinyo za nchi hiyo,” na kuongeza kuwa shinikizo kama hilo litamfanya Macron arudi kwenye mstari.
Trump ametoa matamshi hayo huku kukiwa na lawama na ukosoaji mkali kwa kile kinachoitwa “Bodi ya Amani” kutoka kwa Craig Mokhiber, mkuu wa zamani wa ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR), ambaye alijiuzulu wadhifa wake huo mnamo Oktoba 2023 akipinga vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza na kuungwa mkono na Marekani.
Mokhiber amesema, “Bodi” hiyo “kimuundo na kiutendaji ni upanuzi wa ukaliaji wa mabavu”,na inaashiria uchukuaji wa hatua kuelekea utawala kamili wa kikoloni wa eneo hilo lililowekewa mzingiro.
Katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa X, mkuu huyo wa zamani wa ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema, chombo hicho kinaongozwa na “mmoja wa wahalifu wenza wa mauaji ya kimbari kwa ushiriki wa kimamlaka wa mwingine”, akimaanisha Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel.
Amesisitiza kwamba ukaliaji kimabavu wa Ghaza unafanywa kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kwamba uvamizi huo na mauaji ya kimbari yamevunja kanuni za juu zaidi za sheria za kimataifa.
“Si amri ya kikoloni itokayo kwa Trump, si azimio kali la Baraza la Usalama, na si makubaliano yatakayofikiwa na Serikali ya Mamlaka ya Palestina inayodhibitiwa ambayo yanaweza kuupa uhalali wa kisheria “ukaliaji huo wa ardhi kwa au vita”, ameandika Mokhiber…/