Dar es Salaam. Kwa mara nyingine tena D Voice na Zuchu wanaonyesha kwa nini wanastahili kuwepo WCB Wasafi kwa jinsi wanavyoipambania chapa hiyo kupitia mfululizo wa muziki mzuri kutokea kwao.
Ukimtoa Diamond Platnumz kama mwanzilishi na mmiliki wa WCB Wasafi, Zuchu na D Voice ndio wasanii pekee waliosalia katika lebo hiyo ambayo ilianzia kuwatoa wanamuziki zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Ni hivi karibuni D Voice na Zuchu wameachia wimbo wao mpya, Baridi (2026) uliotayarishwa na Trone ambaye amewahi kuhusika katika nyimbo za Zuchu kama Sukari (2021), Utaniua (2023), Wale Wale (2024) n.k.
Baridi ni wimbo wa mapenzi uliojaa hisia, mvuto na simulizi ya uhusiano uliopamba moto, huku ukinogeshwa na midundo laini na maneno yanayogusa moyo ambayo yanaendana na wanaopenda nyimbo za mapenzi.
Kupitia Baridi, wasanii wote wawili kwa kiasi kikubwa wameonyesha uwezo wa kuzitumia vizuri sauti zao kwa lengo la kuburudisha, sauti ambazo zimepambwa na uandaaji nzuri na wa kisasa wa muziki.
Ndani ya muda mfupi wimbo huo umepata mapokezi mazuri hasa katika majukwaa ya kidijitali ya kusikiliza muziki na ndipo hasa wasanii wengi wameelekeza nguvu kubwa maana soko lenyewe ndiyo hilo.
Tayari umeshika namba moja katika mitandao ya YouTube, Boomplay, Audiomack na Shazam kwa upande wa Tanzania, na unatazamiwa kufika mbali zaidi kimauzo (streams) katika majukwaa mengine.
Ikumbukwe hao ndio wasanii wa mwisho kusainiwa na kutambulishwa WCB Wasafi na Zuchu alitoka mwaka 2020 kupitia Extended Playlist (EP) yake ‘I Am Zuchu’ ambayo ilibeba wimbo maarufu ‘Wana’ uliomtambulisha vizuri.
Kwa upande wake D Voice ambaye alikuwa ameshavuma katika singeli kupitia wimbo wake maarufu, Kuachana Shingapi (2021), yeye alitambulishwa 2023 kupitia albamu yake ‘Swahili Kid’ yenye nyimbo 10.
Swahili Kid ni albamu inayojumuisha aina mbalimbali za muziki ikiwemo Singeli, Bongofleva, Amapiano, Afro Pop na Zouk, huku ikizungumzia kwa kina masuala ya kijamii, mapenzi na changamoto za maisha.
Huku alionyesha kwa uwazi kipaji chake katika uandishi wa nyimbo na uimbaji akiwasilisha ladha mpya na ya kuvutia katika muziki wa Kiswahili, ladha inayoweza kuwagusa na kuwavutia mashabiki wengi.
Wasanii walioshirikishwa katika albamu hiyo ni wale kutokea WCB Wasafi pekee ambao ni Diamond pamoja na Mbosso na Lava Lava ambao kwa sasa hawapo katika lebo hiyo baada ya kuondoka mwaka uliopita.
Pia Zuchu naye alikuwepo ila yeye alipata upendeleo kwa sababu alishirikishwa katika nyimbo mbili – Nimezama na BamBam ambao ndio hasa uliofanya vizuri na kuibeba albamu hiyo.
BamBam ni wimbo namba tatu katika albamu hiyo, huu unazungumzia mapenzi ya dhati ya D Voice kwa mpenzi wake pamoja na dhamira yake ya kutaka kubaki kando yake kwa muda wote kwa sababu anampenda.
Hadi sasa video yake imetazamwa zaidi ya mara milioni 22 YouTube, na muda mrefu ilikuwa ndio wimbo wake uliofanya vizuri zaidi katika mtandao huo kwa muda wote kabla ya kushushwa hadi nafasi ya pili.
Mafanikio ya wimbo huo yalimfanya D Voice kuona ushirikiano wake na Zuchu una faida kubwa na ndipo zikaanza kutoka kazi za pamoja ambazo tayari zimefikia sita ikiwa ni takribami miaka miwili tangu ulipoanza mpapango huo.
Kwa jumla nyimbo ni hizi; BamBam (2023), Nimezama (2023), Nani (2024), Hujanizidi (2024), Baby Mpya (2025) na Baridi na nyimbo za D Voice ni tano, na wa Zuchu ni mmoja (Hujanizidi) kutoka katika albamu yake ya kwanza, Peace and Money.
Kwa matokeo hayo, sasa D Voice amemfikia Bosi wake, Diamond ambaye alikuwa anashikilia rekodi kama mwanamuziki wa kiume aliyeshirikiana na Zuchu mara nyingi zaidi.
Zuchu, mziwanda wa Khadija Kopa, yeye na Diamond wameachia kolabo sita pamoja ambazo ni Cheche (2020), Litawachoma (2020), Mtasubiri (2022), Raha (2024), Wale Wale (2024) na Inama (2025).
Utakumbuka D Voice ni msanii wa nane kusainiwa na WCB Wasafi baada ya Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016), Rich Mavoko (2016), Lala Lava (2017), Mbosso (2018) na Zuchu (2020).