Morogoro. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini), Deus Sangu, amesema Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi umeanza kuleta matokeo chanya katika sekta ya ajira, baada ya kuzalisha maelfu ya nafasi za kazi kwa Watanzania katika kipindi kifupi cha utekelezaji wake.

Sangu amesema hayo Januari 22, 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo mkoani Morogoro, akieleza kuwa mradi huo wa kimkakati unaendana moja kwa moja na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan za kupanua wigo wa ajira kupitia miradi mikubwa ya uzalishaji.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini), Deus Sangu, akizungumza wakati wa ziara katika Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi.

Amesema hadi sasa mradi huo umezalisha ajira za moja kwa moja 1,920 ndani ya kiwanda na mashamba yake, huku ajira zisizo za moja kwa moja zipatazo 8,000 zikitokana na shughuli za usafirishaji, biashara ndogondogo, huduma na shughuli nyingine za kiuchumi zinazozunguka mradi huo.

“Serikali inaona matokeo halisi ya uwekezaji huu kupitia ajira kwa vijana na wananchi wa maeneo ya jirani. Huu ndio mwelekeo wa Serikali – kuhakikisha miradi mikubwa inaleta manufaa ya moja kwa moja kwa jamii,” amesema Sangu.

Kiwanda cha Sukari Mkulazi kinamilikiwa kwa ubia kati ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Jeshi la Magereza kupitia Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza (SHIMA), wawekezaji ambao Waziri aliwapongeza kwa usimamizi wa karibu wa mradi huo.

Mbali na ajira, Sangu amesema mradi huo pia unachochea ukuaji wa uchumi wa eneo la Morogoro na Taifa kwa ujumla kupitia kuongezeka kwa mzunguko wa fedha, mapato ya kodi na kupanuka kwa fursa za biashara kwa wananchi wanaozunguka kiwanda hicho.

Amebainisha kuwa Serikali imewekeza pia katika miundombinu ya barabara zinazounganisha mashamba ya wakulima wadogo wa miwa na kiwanda, hatua inayorahisisha upatikanaji wa malighafi na wakati huo huo kufungua zaidi fursa za ajira na kipato kwa wakulima.

Waziri huyo amesisitiza kuwa ataendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mradi huo ili kuhakikisha unafikia malengo yake, ikiwemo kusaidia kupunguza nakisi ya sukari nchini na kuimarisha zaidi ajira za kudumu na za msimu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni Hodhi ya Mkulazi, Dk Hildelitha Msita, amesema mradi huo umebeba matumaini makubwa kwa wananchi wa eneo hilo, hasa katika ajira na shughuli za kiuchumi.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, amesema taasisi hiyo itaendelea kusimamia uwekezaji huo kwa umakini ili kuhakikisha unaleta faida endelevu kwa wanachama na wakati huohuo kuendelea kufungua nafasi zaidi za ajira.

Naye Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza, Dominic Kazmil, amesema ushirikiano kati ya NSSF na Magereza kupitia SHIMA umeonyesha matokeo chanya, huku ajira zikiwa miongoni mwa mafanikio makubwa ya mradi huo.

Diwani wa Kata ya Mkulazi, Edward William, amesema wananchi wa eneo hilo tayari wananufaika na ajira pamoja na kuongezeka kwa fursa za biashara ndogondogo, hali iliyochochea ustawi wa kiuchumi na kijamii katika kata hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *