Stockholm. Serikali ya Tanzania imezikaribisha nchi za Nordiki kuwekeza katika sekta ya afya nchini, hususan katika maeneo ya tafiti, teknolojia pamoja na uzalishaji wa dawa na vifaa vya tiba.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi, wakati akiwasilisha mada kwenye uzinduzi wa Mkutano wa Afya kati ya nchi za Nordiki na Afrika uliofanyika Januari 22, 2026 jijini Stockholm, Sweden.
Dk Samizi amesema Tanzania iko tayari kuimarisha ushirikiano na nchi hizo kupitia ubadilishanaji wa ujuzi, teknolojia za kisasa na uwekezaji katika viwanda vya dawa na vifaa tiba ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Ameeleza kuwa mkutano huo umejikita katika kujadili masuala ya afya ya uzazi na mtoto pamoja na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, ambayo ni miongoni mwa vipaumbele vya sekta ya afya nchini.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliongozwa na Dk Samizi na ulijumuisha Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Miongoni mwa wataalamu waliohudhuria ni Mkurugenzi Msaidizi wa Afya ya Uzazi na Mama, Dk Mzee Nassoro; Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza na Afya ya Akili, Dk Omary Ubuguyu; Mkurugenzi wa Huduma za Kinga na Elimu ya Afya kutoka SMZ, Dk Salim Slim na Mhadhiri Mwandamizi wa MUHAS, Dk Amani Idris Kikula.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi (wa pili kushoto), akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Huduma za Kinga na Elimu ya Afya wa Wizara ya Afya ya SMZ, Dk Salim Slim (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC), Dk Ntuli Kapologwe wakati wa Mkutano wa Afya kati ya nchi za Afrika na Nordiki uliofanyika jijini Stockholm, Sweden.
Akiwasilisha mafanikio ya Tanzania katika sekta ya afya, Dk Samizi alisema chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu ya afya na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa katika ngazi zote za hospitali.
Alisema kati ya mwaka 2015 hadi 2022, Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000. Aidha, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000, huku vifo vya watoto wachanga vikishuka kutoka 25 hadi 24 kwa kila vizazi hai 1,000.
Kwa upande wao, wawakilishi wa Sweden na Denmark walieleza utayari wa nchi zao kushirikiana na mataifa ya Afrika, ikiwemo Tanzania, kulingana na vipaumbele vya kisera vilivyowekwa na serikali husika.
Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya kundi la Mabalozi Wanawake wa Afrika waliopo katika nchi za Nordiki na taasisi mbalimbali za afya za kimataifa, zikiwemo Maternity Foundation, Dalberg Media, Danish Alliance for Global Health, Global Financing Facility, World Diabetes Foundation, Ferring Pharmaceuticals na Laerdal Global Health.
Viongozi kadhaa wa Serikali za nchi za Nordiki walihudhuria na kuzungumza, akiwemo Waziri wa Afya na Masuala ya Kijamii wa Sweden, Jakob Forssmed; Waziri wa Usawa wa Kijinsia wa Sweden, Nina Larsson; Naibu Waziri wa Afya na Masuala ya Kijamii wa Sweden, Petra Noreback; na Naibu Waziri wa Sera za Maendeleo wa Denmark, Elsebeth Sondergaard Krone. Maafisa waandamizi kutoka Norway na Finland pamoja na mashirika ya kimataifa pia walishiriki.
Kutoka Afrika, mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Afya wa Zimbabwe, Dk Douglas Mombeshora, pamoja na viongozi wa sekta ya afya kutoka Nigeria, Liberia, Rwanda na Kenya. Wengine ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Amref Health Africa, Githinji Gitahi na Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC), Dk Ntuli Kapologwe.
Katika tukio lingine lililofanyika siku hiyo hiyo chini ya mradi wa Goalkeepers unaofadhiliwa na Mfuko wa Gates, Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark, Lars Løkke Rasmussen na Bill Gates walihudhuria na kuzungumza.
Akizungumzia mchango wa sekta binafsi, Gates alisema taasisi binafsi zina nafasi muhimu katika kuimarisha sekta ya afya duniani, hususan katika kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto pamoja na kuharakisha kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).